Habari

Wangamati aagiza baa zifungwe Bungoma siku ya sensa

August 13th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

BAA katika Kaunti ya Bungoma zitafungwa katika usiku wa Agosti 24-25 ili wenyeji wawe nyumbani kwa ajili ya kuhesabiwa katika shughuli ya kitaifa ya sensa, amesema Gavana.

Gavana Wycliffe Wangamati amewataka wenye baa katika kaunti hiyo kujiandaa na kutii agizo la kufungwa kwa biashara hizo.

Vyombo vya kudumisha usalama vimetakiwa kuhakikisha baa zinafungwa kuanzia saa kumi na mbili jioni Agosti 24 kama njia mojawapo ya kuhakikisha wenyeji wanapatikana majumbani mwao kuhesabiwa.

“Sensa ya mwaka 2019 ni muhimu kwa sababu itatoa takwimu muhimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo, usimamizi, ugavi wa raslimali pamoja na taswira faafu zaidi ya mipaka ya asasi za kiutawala nchini. Wakazi wanafaa wawe nyumbani ili tujue idadi kamili ya watu walio Bungoma,” alisema Bw Wangamati.

Aliyasema hayo Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) mjini Kakamega katika Kaunti ya Kakamega ambayo inapakana na yake.

Sensa Kenya hufanyika kila baada ya miaka 10.

Mwaka huu Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) linaendesha shughuli hiyo kwa utaratibu wa kidijitali.

Sensa za awali zilifanyika 1948, 1969, 1979, 1989, 1999 na mwaka 2009.