MakalaSiasa

WANGARI: Kibra waheshimu Okoth kwa kuchagua mchapakazi

September 19th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

SIASA za Kenya huwa zimejaa vituko. Ni vigumu wiki kupita bila kusikia kisanga cha kustaajabisha, kuchekesha na hata wakati mwingine kuudhi.

Iwapo wabunge hawavurumishiani makonde na mateke bungeni, wanamkejeli na kumzomea spika, iwapo hawaungani pamoja kupigia debe kujiongezea mishahara minono, basi wabunge wanaume wanaungana kumfukuza mbunge mwanamke kwa kuingia bungeni na mtoto wake mchanga.

Katika siku za hivi majuzi, tumeshuhudia sarakasi tele kuhusiana na uchaguzi mdogo wa kumchagua mrithi wa marehemu Mbunge wa Kibra Ken Okoth.

Vitimbi vyote hivyo vilianza wakati DJ maarufu Chrispinus Odhiambo almaarufu kama Kriss Darlin alimpigia magoti Raila Odinga, akimtaka ampe baraka zake kugombea kiti hicho.

Hata kabla ya Wakenya kushusha pumzi kutokana na kitendo hicho kisicho cha kawaida, viongozi kadha wa vyama mbalimbali walijitokeza kuwapigia debe wagombeaji ambao wamewaacha Wakenya vinywa wazi.

Jubilee ilijitokeza na mchezaji soka nyota aliyestaafu MacDonald Mariga ambaye ameandamwa na misururu ya visanga kuanzia kutojisajilisha kama mpiga kura na cha ajabu zaidi, kushindwa kuamua kuhusu umri wake ambapo hana uhakika iwapo alizaliwa 1981 au 1987!

Endapo Wakenya walifikiri walikuwa wameona makubwa, kiongozi wa Wiper naye alijitokeza na kutangaza rapa maarufu Jackson Makini almaarufu CMB Prezzo angewania kiti hicho kwa tiketi ya Wiper, lakini kwa haraka akaghairi nia na kutanga kwamba msanii huyo machachari angegombea wadhifa huo 2022.

Ni jambo la kuvunja moyo kuona kumbukumbu ya marehemu Okoth aliyekuwa kiongozi wa kupigiwa mfano kutokana na rekodi yake ya miradi ya maendeleo katika eneobunge lake, ikifanyiwa masihara ya kila namna.

Okoth alitimiza mengi kwa muda mfupi mno kushinda viongozi kadha ambao wamekuwa katika nyadhifa za uongozi kwa miongo mingi. Inatamausha hata zaidi kufikiria kuhusu hatima ya wakazi wa Kibra eneo lao linapogeuzwa uwanja wa sarakasi za kisiasa ambapo kila upande unavutia upande wake.

Hata katika mitandao ya kijamii, hali ni ileile huku baadhi ya Wakenya wakishangaa ni lini siasa za Kenya zilianza kutilia maanani elimu, maadili au ujuzi ili kuchagua kama kiongozi.

Taswira hii ya kuvunja moyo ndiyo uhalisia wa jinsi viongozi wanavyochaguliwa bila kuzingatia sifa muhimu. Kwa vyovyote vile, heshima ya mwisho na muhimu tunayoweza kumpa Okoth ni kuhakikisha kiongozi atakayemrithi Novemba 7, ni mchapa kazi kama yenye tu.