WANGARI: Mabadiliko katika NHIF yawe ya kumfaidi mwananchi

Na MARY WANGARI

KATIKA miezi michache ya hivi karibuni, serikali imekuwa ikijitahidi kufanyia mageuzi muhimu Bima ya Kitaifa kuhusu Afya Nchini (NHIF), katika juhudi za kuboresha huduma za afya nchini.

Mojawapo wa mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa mfumo wa kuwasajili kielektroniki wanachama 8.9 milioni wa NHIF kwa kutumia alama zao za vidole.

Mfumo huo mpya ambao tayari umeanzishwa katika hospitali za Kaunti za Nairobi, Eneo la Kati, Magharibi, Nyanza, Mashariki na Bonde la Ufa, unadhamiriwa kukomesha udanganyifu na kuboresha malipo ya huduma za matibabu.

Aidha, kuna Mswada wa Kufanyia Marekebisho Bima ya Kitaifa kuhusu Huduma za Hospitali unaopendekeza kuifanya kuwa lazima kwa kila mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kujisajilisha kama mwanachama wa NHIF, miongoni mwa mageuzi mengine.

Juhudi hizi zinastahili kupongezwa na zinaashiria siku njema za usoni.

Kando na umuhimu wa afya njema katika kufanikisha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ambao ni mojawapo wa Ajenda Kuu za Maendeleo Duniani, uhalisia ni kwamba, ili taifa lolote liweze kuendelea, ni sharti raia wake wawe wazima kiafya.

Serikali hivyo basi, ni sharti ihakikishe utekelezaji kikamilifu wa sera zitakazowezesha kuwepo kwa huduma bora za afya kwa bei nafuu ambayo kila raia anaweza kuimudu.

Njia mojawapo ya kufanikisha haya ni kupitia ushirikiano wa serikali na mashirika ya kibinafsi yanayotoa huduma za bima ya afya ili kuboresha huduma ya afya nchini kupitia miundomsingi thabiti na vifaa vya matibabu.

Kwa muda mrefu, Wakenya wamejipata taabani baada ya kulemewa na mzigo wa kugharimia matibabu huku wengi wao wakifilisika hata baada ya kujisajili na bima za umma kama vile NHIF.

Si ajabu kwamba wengi wanaojiweza kifedha, wamekimbilia mashirika ya kibinafsi yanayotoa bima za afya wakiwa na hakikisho la kupata huduma bora zaidi japo kwa ada ghali.

Hali kwamba NHIF imekuwa ikibadilisha sheria zake mara kwa mara hata bila ya wanachama wake kutarajia inafanya mambo kuwa magumu hata zaidi.

Mabadiliko sharti yamfaidi mwananchi wa kawaida kinyume na kumwongeza mzigo zaidi.

Ili NHIF iwe na manufaa kwa Wakenya, ni sharti serikali ihakikishe kwamba mageuzi yanayoendelea kamwe hayatahujumu hatua zilizopigwa katika kuboresha bima hiyo ya kitaifa kuhusu afya.

Ni kupitia tu kuwepo kwa wananchi walio wazima kiafya ndipo tunaweza kuunda taifa imara katika kila nyanja.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii