Makala

WANGARI: NASA yafaa ielekeze nguvu zake katika siasa za ustawi

February 14th, 2018 2 min read

Vinara wa NASA Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wakihutubu. Picha/ Maktaba

Na MARY WANGARI

KATIKA mahojiano ya dakika tatu na BBC wiki iliyopita, kiongozi wa NASA Raila Odinga alitaka uchaguzi mpya ufanyike kufikia Agosti lakini akakana njama za kuongoza mapinduzi ya serikali.

Hamna shaka kwamba kiongozi huyo wa upinzani, na muungano wake wa kisiasa, ana masuala ambayo hayajatatuliwa na mara kwa mara wameeleza malalamishi yao kuhusu mchakato wa uchaguzi uliosababisha marudio ya uchaguzi mwaka jana.

Hata hivyo, inasikitisha kwamba Raila yamkini anaelekeza malalamishi yake kwa watu wasiofaa. Madai ya uchaguzi mpya yamekuwa mojawapo ya mbinu ambazo yeye na vinara wenzake wa NASA wamekuwa wakitumia kuihangaisha serikali ya Jubilee.

Lakini ni kana kwamba kinara mwenza wa NASA anachukua mkondo tofauti, ambapo katika mkutano wa hadhara hivi majuzi alihimiza kuwepo kwa mjadala kati ya upinzani na Rais Uhuru Kenyatta, ili “kupunguza joto la kisiasa”.

 

Walakini

Wakati muungano kama NASA unapojitwika jukumu la kushinikiza uchaguzi mpya miezi michache tu baada ya mapambano makali ya siasa ambapo watu walitoa uamuzi wao, inadhihirisha bayana kuwepo kwa walakini fulani.

Kwingineko, matamshi kama yale ya Moses Wetangula yanarejesha Wakenya katika mazingira ya uchaguzi, jambo ambalo halifai kabisa.

Matamshi hayo yalisababisha wawekezaji kurefusha muda wao wa ‘kungoja na kuona’, ulioathiri kiasi uchumi mwaka jana kufuatia kucheleweshwa kwa uwekezaji wenye thamani ya mabilioni.

Jinsi tunavyofahamu, mwaka 2017 Kenya ilipitia kipindi kigumu cha kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu Agosti, uchaguzi wa marudio uliofuatia Oktoba 25 pamoja na kesi kali za uchaguzi.

Ni dhahiri kwamba taifa linahitaji mno kuondokewa visanga vya kisiasa kama vile vinavyoonyeshwa na upinzani na kujishughulisha na maendeleo ya kitaifa.

 

Waepuke ubinafsi

Iwapo kweli NASA ina nia njema kwa taifa, viongozi wake sharti waepukane na mwelekeo wa kibinafsi wa siasa unaojisawiri kuwa kisingizio cha kujali maslahi ya wananchi.

Wakati umewadia kwa siasa kali na wanaoziendeleza kusalia nyuma ili kuwezesha taifa kusonga mbele.

Ni muhimu kukumbuka kwamba, huku upinzani ukiwa na nafasi ya kuchangia katika demokrasia, shughuli hiyo ifanywe kwa kujali maslahi ya wananchi ambao ndio wakuu.

Ikiwezekana, kuifanya serikali iliyopo kuwajibika pasipo kugeukia visanga visivyo na manufaa na kulalamika kila uchao.

Ni muhimu kwa upinzani kukomesha msimamo wake wa kundi la wapiganaji na badala yake kugeukia siasa zenye mwelekeo unaojali maslahi ya wananchi ili kuwezesha manufaa ya kila mwananchi kwa jumla.