Makala

WANGARI: Sera zibuniwe kuadhibu wanaotumia mitandao vibaya

November 7th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MAJUZI, aliyekuwa rais wa Amerika Barack Obama alikashifu kizazi cha leo kinachotumia vibaya mitandao ya kijamii kudhalilisha na kuwavuta wengine chini kwa kutoa shutuma kiholela ili tu kuonekana kama waliopevuka kisiasa.

Obama alitahadharisha vijana wanaowahukumu wengine mitandaoni ili tu wajihisi vyema nafsi zao, akiwaonya kwamba hawataenda mbali maishani.

Kauli ya rais huyo iliashiria tu kijisehemu tu cha jinsi mitandao ya kijamii inavyotumiwa vibaya na baadhi ya watu katika jamii ya leo.

Inashangaza kuona jumbe zinazochapishwa zilizojaa matusi na chuki.

Hatuwezi hata kukisia kiwango cha kuathirika kisaikolojia kwa familia ya marais waliostaafu Daniel Moi na Mwai Kibaki baada ya watu fulani kujitia jukumu la kuamua ni nani anayeishi au kufariki na kuanza kueneza tetesi kuwa walikuwa wameaga dunia.

Baadhi hata walianza kujiandaa kwa sikukuu kana kwamba walikuwa na uwezo wa kujua ya kesho. Ni dhahiri kuwa unyama umewatoka wanyama na kuwaingia binadamu katika kizazi cha leo cha kidijitali.

Kando na kuwa ni viongozi wanaoenziwa, wazee hao pia wana familia zao zinazowapenda na ambazo zinaomba Mungu kutwa kucha kuwahifadhi wapendwa wao. Japo mauti ni hatima ya kila mwanadamu, ni ukatili usio kifani na ukosefu wa maadili kumtakia kifo mwingine kwa kuwa hakuna ajuaye ya kesho.

Watu kadha wamesimulia jinamizi walilopitia baada ya kushambuliwa vibaya mitandaoni ambapo hata baadhi ya wahasiriwa wamejitoa uhai kutokana na kuathirika kisaikolojia.

Ukweli ni kuwa, wanaoendeleza uovu huu ni waoga wanaojificha nyuma ya tarakilishi au rununu zao.

Aghalabu, watu hawa huwa na machungu au wamekata tamaa maishani na hivyo hutumia kila fursa kuwadunisha wengine na kuwafanya wajishuku au kujichukia ili wawe katika viwango sawa na wahuni hao.

Japo mitandao ya kijamii imejaribu kwa upande wake kusitiri watu kutokana na dhuluma za kidijitali kwa kuimarisha usalama, sera mwafaka zinapaswa kubuniwa kwa dharura ili kuwaadhibu vikali wahuni wanaotumia mitandao ya kijamii kuwadhuru wengine kisaikolojia kwa kueneza habari za uongo au kuwaharibia sifa.