Makala

WANGARI: Sheria za mitandaoni ziwepo kudhibiti nyimbo kama ‘Wamlambez’

September 11th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MWENYEKITI wa Bodi ya Filamu Nchini (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua majuzi aliibua hisia mbalimbali kufuatia pendekezo lake la kudhibitiwa kwa uchezaji wa nyimbo zinazovuma ‘Wamlambez’ ya Sailors na ‘Tetema’ ya wasanii nyota wa Bongo Diamond na Rayvanny.

Kulingana naye, nyimbo hizo zinafaa kuchezwa tu kwenye baa na vilabuni usiku na wala si katika maeneo ya hadhara ambapo watoto wanaweza kuwepo kutokana na maudhui ya ngono yanayonuizwa.

Pendekezo lake lilipokelewa kwa kiwango sawa cha kashfa na pongezi na kama ilivyotarajiwa, umaarufu wa vibao hivyo hasa ‘Wamlambez’ ambacho kimevuma sana katika siku za hivi majuzi kiasi cha kutamba kimataifa, ulipaa zaidi badala ya kushuka.

Watu zaidi hata ambao hawakujishughulisha nacho mbeleni walijitosa kwenye mtandao wa Youtube kwa hamu ya kutaka kujua kibao hicho hasa kinahusu nini kiasi cha kukatazwa kuchezwa hadharani?

Jinsi tunavyojua haramu ni tamu, na hivyo ndivyo vibao hivyo viwili na vingine vingi vinavyopigwa marufuku kutokana na ukiukaji wa maadili, vinavyozidi kubobea licha ya kukatazwa.

Ni wazi kwamba hakuna haja ya kupiga marufuku kazi fulani ya usanii kwa lengo la kuhifadhi maadili katika jamii, ilhali wanajamii wanaweza kuipata kirahisi mitandaoni wakati wowote bila kujali umri au jinsia.

Katika enzi hii ya utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kinachohitajika kwa dharura ni kubuniwa kwa sheria na sera thabiti zinazodhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuwalinda wananchi dhidi ya matini zisizofaa.

Inahofisha kwamba mitandao ya kijamii imekosa kudhibitiwa kabisa nchini ambapo hata watoto wanaweza kupata kirahisi filamu na nyimbo za ngono, kujiunga na makundi ya kishetani, kufahamu jinsi ya kujiua au kutekeleza mauji na machukizo mengine, kupitia tovuti na mitandao mbalmbali.

Si ajabu kwamba matokeo yake ni kuongezeka kwa visa vya kushtusha tunavyoshuhudia kila kunapokucha.

Mapema mwaka huu, kulikuwa na ripoti kuhusu baadhi ya vibonzo vya watoto kwenye mtandao wa kijamii wa Youtube, vilivyosheheni vidokezo vya kuwaonyesha watoto jinsi ya kujitia kitanzi.

Ni vigumu hata kukisia kiwango cha athari kisaikolojia kwa watoto waliokuwa na bahati mbaya ya kutazama vipindi hivyo, ikizingatiwa kuwa, watu wengi wanaamini vibonzo ni vipindi salama kwa watoto.

Ili kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii, ni sharti kubuniwe sheria na sera madhubuti dhidi ya mashirika ya teknolojia ili kuyashinikiza kuwajibika katika kuwalinda watumiaji wake dhidi ya mambo yanayoweza kuwadhuru. Aidha, mashirika yanayokiuka sheria hizo yanapswa kuchukuliwa hatua kali kisheria ili kuhifadhi maadili katika jamii.