Makala

WANGARI: Teknolojia mpya suluhu kwa changamoto za karne hii

January 2nd, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

BAADA ya mbwembwe na shamrashamra za kuaga 2019 na kukaribisha Mwaka Mpya wa 2020, pana haja kubwa ya kutilia maanani nafasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kujiendeleza kama taifa na bara la Afrika kwa jumla.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo ulimwengu tayari umeshuhudia katika karne iliyopita, bila shaka tunaweza tu kutarajia makubwa hata zaidi hasa katika tasnia ya teknojia.

Katika karne iliyopita, ulimwengu ulipiga hatua kuu kufuatia ujio wa utandawazi, mitandao ya kijamii ambayo kwa hakika imegeuza ulimwengu kuwa kijiji kidogo tu na kuwaunganisha binadamu kote duniani. Mataifa yaliyoendelea tayari yamegundua umuhimu wa teknolojia katika kizazi hiki na yako mstari wa mbele kuitumia katika nyanja mbalimbali.

Matumizi ya teknolojia katika kuunda silaha za kivita ili kujihami na kuimarisha usalama, kwenye ulingo wa tiba na sayansi ili kutibu maradhi sugu kama Ebola na saratani, usafirishaji kielektroniki, mawasiliano kimitambo, elimu, maarifa kupitia mashine ni baadhi ya ufanisi uliofanikishwa na teknohama.

Huku haya yakijiri, litakuwa jambo la kusikitisha endapo Kenya na Bara la Afrika kwa jumla litasalia nyuma kwa kukataa kutembea na majira. Kwa hakika, ni teknolojia tu itakayowezesha Kenya na Afrika kukabiliana vilivyo na masaibu mbalimbali yanayokumba bara hili na ambayo huenda hata yakaongezeka 2020.

Majanga kama vile ukame, mafuriko, mikurupuko ya maradhi mbalimbali, misongamano ya trafiki inayolemaza usafiri na kuathiri uchumi, ukosefu wa ajira na mengineyo ni mifato ya masuala yanayoweza kulainishwa kupitia teknolojia.

Isitoshe, ishara ambazo tumekuwa tukishuhudia hivi majuzi kuhusiana na mabadiliko ya hali ya anga ambayo yamesababisha majanga ya kuhofisha, ni ithibati tosha kuwa tunahitaji kufikiria kuhusu kawi mbadala badala ya kuegemea mbinu za jadi. Serikali tayari imeanzisha juhudi za kushirikisha teknohama katika mfumo wa elimu nchini. Vifaa kama vile tarakilishi, vipakatalishi na vinginevyo vinaweza kuboresha masomo na kuwawezesha wanafunzi kujihami ipasavyo kukabiliana na changamoto zinazowasubiri katika kizazi hiki cha kidijatali.

Aidha, kujumuisha teknolojia katika mfumo wa elimu huchochea ubunifu miongoni mwa wanafunzi binafsi hivyo kupiga jeki uvumbuzi zaidi wa kiteknolojia.

Ni wazi kuwa mataifa yatakayomudu mabadiliko katika karne hii mpya ni yale ambayo yatawekeza katika teknolojia kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Natumai wadau husika wataharakisha utekelezaji wa elimu kidijitali kwa kutoa mafunzo na miundomsingi inayohitajika ili kuwawezesha walimu na wanafunzi kujihami vilivyo.