Makala

WANGARI: Uzalishaji kawi salama utaharakisha ustawi wa nchi

July 22nd, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

HUKU muda wa kufanikisha malengo ya Ruwaza 2030 ukizidi kuyoyoma, pana haja ya kutilia maanani suala la kuwezesha kuwepo kwa kawi safi na salama kuhusiana na mazingira, yenye bei nafuu na inayoweza kutegemewa katika sekta zote.

Suala hili haliwezi kusisitizwa vya kutosha ikizingatiwa nafasi muhimu ya kawi katika kufanikisha nyanja zingine za ustawishaji kama vile elimu, huduma bora za afya, miundomsingi na miji ya kisasa miongoni mwa huduma zingine.

Kenya sawa na mataifa mengine duniani, imepania kufanikisha malengo yake ya maendeleo kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kuwekeza katika kawi inayofaa.

Serikali imepiga hatua kubwa kufikia sasa huku ikijikakamua kuwekeza katika miradi ya kawi ili kuhakikisha Wakenya zaidi wanafurahia nguvu za umeme.

Hata hivyo, juhudi zaidi zinahitajika iwapo ndoto ya kufanikisha Ruwaza 2030 kuhusu Ustawishaji wa Malengo ya Maendeleo (SGD), ambayo inategemea pakubwa sekta ya kawi, itafanikiwa.

Kauli hii inathibitishwa na ripoti ya pamoja iliyotolewa mapema mwaka huu katika utafiti uliofanywa na mashirika kama vile Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo, Benki Kuu ya Dunia, Shirika la Afya Duniani na Shirika la Kawi Kimataifa.

Kutokana na hayo, ni dhahiri kuwa serikali na wadau ni sharti watilie maanani sekta ya kawi salama inayozingatia uhifadhi wa mazingira.

Kuna mwanga wa matumaini hata hivyo huku data iliyokusanywa na Shirika la Kawi Kimataifa (IEA) ikiorodhesha Kenya miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa matumizi ya kawi safi ulimwenguni.

Aidha, data hiyo inaashiria kwamba, kiwango cha usambazaji wa umeme nchini kimeongezeka pakubwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita na kufikia asilimia 75 nchini.

Bila shaka, hizi ni ripoti za kutia moyo ikizingatiwa kwamba, asilimia 86 ya kawi nchini inatokana na chemichemi salama kuhusiana na mazingira, ikiongozwa na umememvuke kupitia kampuni ya uzalishaji ya KenGen.

Kawi kutokana na upepo na jua vilevile ni sehemu ya uwekezaji katika kawi salama ambayo bila shaka itapiga jeki nafasi ya Kenya kwenye ramani ya ulimwengu kuhusiana na viwango vya kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Isitoshe, ili kuthibitisha azma yake kuhusiana na kawi salama, serikali tayari imewekeza kitita cha Sh140 bilioni ambacho ndicho cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya Kenya kuhusiana na uwekezaji katika kawi safi.

Ili Kenya itimize kikamilifu malengo yake kuhusu ukuaji wa uchumi, ni sharti serikali ijikakamue kufanikisha mradi wa Awamu ya Mwisho kuhusu Mamlaka ya Umeme Mashinani utakaowezesha maendeleo katika sekta zote nyingine.

[email protected]