Makala

WANGARI: Vyombo vya habari Magharibi vikome kuisawiri Afrika kwa njia ya ubaguzi

November 4th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

RAIS John Pombe Magufuli aliibuka mshindi hivi majuzi katika kinyang’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali na kuangaziwa pakubwa na jamii na vyombo vya habari kimataifa.

Kwa jumla, shughuli ya uchaguzi nchini humo ilifanyika kwa amani sawa na historia ya chaguzi katika taifa hilo, linaloangaziwa kama mhimili wa uthabiti Barani Afrika.

Hata hivyo, matukio hayo yalikuwa tofauti kabisa na taswira iliyoashiriwa na waangalizi, mashirika na vyombo vya habari kimataifa.

Tasnia za habari kimataifa zilimsawiri Magufuli kama kiongozi wa kiimla aliyewaponda wapinzani wake, kunyamazisha wanahabari nchini humo na kuwatia woga Watanzania ambao hawakuwa na hiari ila kuvumilia miaka mingine mitano chini ya uongozi huo.

Vituo hivyo vilimpigia debe mpinzani mkuu wa Magufuli ambaye pia ni kiongozi wa upinzani Tundu Lissu kiasi cha kudai kuwa njia pekee ambayo rais huyo angeibuka mshindi ni kupitia udanganyifu.

Ripoti hizo hazikuashiria uhalisia wa kisiasa Tanzania kulingana na wachangunzi nchini humo.

Hali kwamba shughuli za kampeni na uchaguzi nchini Tanzania zilifanyika wakati sawa ambapo Rais wa Amerika Donald Trump alikuwa akiwania hatamu ya pili huku akikabiliwa na ushindani mkali vilevile, haikutosha kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia ripoti zenye usawa bila ubaguzi dhidi ya Afrika.

Licha ya marais Magufuli na Trump kuwa na sifa nyingi zinazofanana, mashirika ya habari ya Magharibi yaling’ang’ania kumkashifu rais wa Tanzania na kumsawiri kihasi huku yakionekana kunuiza tu kuhusu Trump.

Kando na kudai kwamba njia pekee ambayo mpinzani wake Joe Biden angembwaga katika uchaguzi ni kupitia wizi wa kura, na hata kumwelekeza Mwanasheria Mkuu nchini humo kumchunguza na kumshtaki Biden, Trump pia alikataa kutia sahihi mkataba wa kuondoka mamlakani kwa njia ya amani endapo angepoteza kiti chake.

Ni kinaya kikuu basi kwamba vyombo vya habari kimataifa, ambavyo baadhi vimewahi kutaja Afrika kama bara lisilokuwa na matumaini, vinaweza kufikirwa hata kwa dakika moja kuwa vinajali kwa dhati mustakabali wa siasa Afrika.

Kampeni za kisiasa zilizohusisha Magufuli na Trump ni mfano thabiti wa uhalisia huu wa kutamausha.

Kwa muda mrefu, Afrika imekuwa ikisawiriwa visivyo na vyombo vya habari vya kimagharibi visivyochelea kutia chuku matukio mabaya huku vikidunisha ripoti za ufanisi barani humu.

Hata hivyo, enzi ambazo tasnia ya habari ya Magharibi ilitumika kueneza kasumba potovu dhidi ya Afrika kupitia ushahidi finyu, ripoti zenye mapendeleo na makala hasi ya uhariri, zimepitwa na wakati.

Wakati umewadia kwa vyombo vya habari barani Afrika kujitokeza na kutoa taswira halisi ya Afrika kwa ulimwengu kupitia simulizi za kweli zinazoashiria ukweli halisi bila ubaguzi, chuki wala shinikizo hasi.

[email protected]