Dondoo

Wang'atwa na nyuki wakila uroda

March 30th, 2020 1 min read

NA JOHN MUSYOOKI

MBIUNI, MACHAKOS 

KIOJA kilishuhudiwa hapa, jombi na kimada wa mtaani walipovamiwa na nyuki wakirushana roho ndani ya kichaka.?

Duru zinasema kwamba jamaa huyo anapenda vichuna wa mtaani kupindukia na alikuwa akiwateka bila kubagua.

Siku ya kioja mwendo wa jioni hivi, jamaa aliondoka na demu kilabuni kama ilivyokuwa desturi yake. Yadaiwa wawili hao walipofika karibu na shamba la mkulima mmoja anayefuga nyuki, polo na demu walipandwa na mzuka na wakatulia kwenye kichaka kilicho karibu.

Wawili hao walianza vituko vyao vya kulishana uroda bila kujali kabla ya starehe zao kuharibiwa na jeshi la nyuki.

Inasemekana baada ya muda mfupi wawili hao walisikika wakipiga nduru huku kila mmoja akiomba usaidizi baada ya kuvamiwa na nyuki hao.

‘Uuuiii! Njooni mtusaidie. Tutauawa na nyuki hawa,’ jamaa alipiga nduru huku demu akijaribu kuwafukuza nyuki hao bila kufua dafu.

Majirani waliokuwa karibu walivutiwa na kamsa hiyo na wakaenda kujua kilichokuwa kimejiri.

Watu walipigwa na butwaa walipowapata wawili hao wakijaribu kuvaa mavazi yao huku nyuki wakiendelea kuwashambulia.

‘Kwani nyuki hawa wametoka kuzimu? Wametuharibia starehe zetu hapa,’ demu alisema aliyekuwa mlevi alisema.

Wakati huo mwenye shamba alifika na kuanza kuwafokea wawili hao kwa kufanya shamba lake kuwa danguro.

‘Nani aliwapatia ruhusa ya kuingia shambani kwangu bila ruhusa? Hapa huwa ninafuga nyuki na kuna mizinga karibu,’ mwenye shamba alisema.

Hata hivyo, nyuki walizidi kuleta fujo na kung’ata kila mtu aliyekuwa karibu akiwemo mwenye kuwafuga.

Ilibidi kila mmoja kutimua mbio kujiokoa.