Habari MsetoSiasa

Wania urais 2022, mawaziri wa zamani wamshauri Gideon Moi

February 10th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

VIONGOZI waliohudumu katika serikali ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi sasa wanamtaka mwanawe Seneta wa Baringo Gideon Moi kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi hao waliokuwa wakizungumza walipoenda kufariji familia ya Mzee Moi nyumbani kwake, Kabarnet Gardens, jijini Nairobi, walisema Seneta wa Baringo anafaa kuendeleza uongozi bora wa baba yake kwa kuwania urais katika uchaguzi ujao.

“Wewe ndiye umeachiwa jukumu la kuendeleza chama cha Kanu. Hatutaki kukuona ukiwania useneta tena katika uchaguzi ujao,” akasema Maalim Mohamed aliyekuwa waziri katika serikali ya Moi kati ya 1983 na 2002.

“Mimi ningali mwanachama wa Kanu na tutakuunga mkono,” akaongezea.

Bw Mohamed ambaye pia alikuwa mbunge wa Garissa kati ya 1979 na 2002, alisema kuwa ndoto ya Mzee Moi kutaka chama cha Kanu kutawala kwa miaka 100 itatimia kupitia kwa Seneta Gideon Moi.

Waziri huyo wa zamani alimtaja Mzee Moi kama kiongozi ambaye hakubagua Wakenya kwa misingi ya kikabila.

Naye Bw Barua Chele aliyehudumu kama Katibu wa Wizara ya Serikali za Mitaa katika serikali ya Moi, alisema Bw Gideon Moi hana budi kufuata nyayo za baba yake aliyejitolea kwa hali na mali kuunganisha Wakenya.

“Tunatarajia kwamba utafuata nyayo za baba yako kwa kuwania urais. Mtoto wa nyoka ni nyoka,” akasema Bw Chele.

Wengine waliotoa kauli sawa na hizo ni aliyekuwa waziri wa Vyama vya Ushirika John Cheruiyot na waziri wa zamani Julia Ojiambo.

Prof Ojiambo alikuwa ameandamana na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Stephen Kiama na Chansela wa chuo hicho Vijoo Rattansi.

“Tumekuja hapa kuleta rambirambi zetu kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Nairobi,” akasema Prof Ojiambo.

Kwa upande wake, Seneta wa Baringo aliwashukuru Wakenya ambao wamekuwa wakimiminika Bungeni, nyumbani kwao Kabarnet Gardens (Nairobi) na Kabarak (Nakuru) kuwafariji.

“Nawashukuru Wakenya kwa kufika kutufariji. Upendo wenu daima utakumbukwa,” akasema Bw Gideon Moi alipokuwa akihutubia wageni waliofika kufariji familia yake katika jumba la Kabarnet Gardens.

Tofauti na Naibu wa Rais William Ruto ambaye ametangaza azma yake ya kutaka kuwania urais 2022, Seneta Moi amesalia kimya.