Michezo

Wanjie na Mueni wanyamazisha wapinzani wao urushaji vishale

June 25th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WARUSHA vishale Peter Wanjie (AP) na Pascalina Mueni (Mang’ Darts) waliibuka mabingwa wa taji la Makavazi Cup baada ya kutesa katika fainali kitengo cha mchezaji mmoja mmoja  zilizochezewa ukumbi wa Qunu Garden Resort, Chuka.

Peter Wanjie alitwaa ubingwa wa mpambano huo ulioandaliwa kwa mara ya kwanza kabisa alipomchoma Muthunga Muiruri wa Nairobi Stima, seti 5-2 katika fainali. Naye Pascalina Mueni alitawazwa malkia baada ya kumzaba Rosemary Wangui (Blue Triangle) seti 5-4 kwenye mechi ya kusisimua si haba.

”Binafsi sikufahamu jinsi nilipata ujasiri na kuwabwaga washiriki wengine wote kwenye pambano hilo,” Pascalina Mueni alisema na kudai kuwa kamwe haikuwa mteremko.

William Mbogo (Nairobi Stima) na Beneka Mwololo (Museum) kila mmoja alivishwa ushindi wa tatu bora baada ya kuvuna seti 3-2 na 3-0 dhidi ya Wycliffe Omariba (Mang’) na Priscar Ongwora (Matumbo) mtawalia.

Kitengo cha wanaume, Nelson Nyakundi (Nairobi Stima) aliibuka bora kwa kuchapa alama 180 mara nne, huku mwenzake Peter Kirimi akibeba ubingwa wa kupiga alama nyingi kuliko wote alipovuna pointi 160 kwa kutumia mshale mmoja.

Kadhalika mchezaji wa Museum, Phyllis Murugi aliibuka malkia wa kipute hicho alipoonyesha ustadi tosha kwa kupiga alama 180 mara mbili na kuwapiku wapinzani wengine.

Kwenye nusu fainali, Peter Wanjie alipiga William Mbogo seti 4-3 huku Muthunga Muiruri akizoa idadi sawa na hiyo mbele ya Wycliffe Omariba. Kwa wanawake, Pascalina Mueni alishinda Priscar Ongwora seti 4-1 naye Beneka Mwololo alizabwa seti 4-0 na Rosemary Wangui.