Habari za Kitaifa

Wanjigi aitaka jamii ya Dholuo kuendea urais au unaibu rais 2027

April 7th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa Chama cha Safina, Jimi Wanjigi ameitaka jamii ya Dholuo isikubali chochote isipokuwa nafasi ya Rais au Naibu Rais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Wanjigi pia amehimiza jamii hiyo kuchukua msimamo thabiti kuhusu matakwa ya jamii hiyo mirengo ya kisiasa itakayotafuta kiti cha urais wa 2027 itakapokuwa ikisukwa.

Akizungumza Jumamosi, Aprili 6, 2024 katika Kaunti ya Migori, Wanjigi alisema jamii hiyo inafaa kuhusishwa katika meza ya uundwaji wa serikali ijayo kama jamii zingine.

“Kama jamii ya Ziwa Victoria, mnafaa kuweka bayana watakwa yenu yasiyoweza kupunguzwa.Tuketi. Tutengeneze meza hiyo. Ikiwa hatuwezi kupata urais, basi iwe wa naibu wa rais,” Bw Wanjigi alisema alipohudhuria hafla ya mchango katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Ogengo katika eneobunge la Nyatike.

Mwanasiasa huyo alitumia fursa hiyo kukosoa utawala wa kenya Kwanza.

Alipinga safari za mara kwa mara za Rais William Ruto Ughaibuni na kudai kwamba kiongozi  huyo wa nchi ameshindwa kutimiza ahadi nyingi za kampeni ambazo aliahidi Wakenya, haswa wale wa tabaka la chini, ambao aliwaita mahasla.

“Tuna Rais asiyekuwepo. Mtu ambaye ameketi kwenye kiti cha enzi anajua kwamba hii ni meli inayozama. Kwa hivyo anasafiri kila wakati. Unasikia leo yuko hapa, kesho yuko huko Ulaya. Hebu niambie, mtu huyo si amekata tamaa tayari?” Bw Wanjigi aliuliza.

Aliandamana na magavana Ochilo Ayacko (Migori), Anyang Nyong’o (Kisumu), Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, Mbunge wa Nyatike Tom Odege miongoni mwa viongozi wengine.

Kinyume na Septemba 2021, alipopokea mapokezi ya fujo huko Migori alipokuwa akijipigia debe kwenye azma yake ya urais, Bw Wanjigi alikaribishwa kwa furaha na kukumbatiwa wakati wa hafla hiyo ya kanisa.

Gavana Ayacko alimwambia Bw Wanjigi aendelee kuzuru Migori na baraka za kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kuna wakati ulitembelea eneo hili na watu wachache wakakunyanyasa. Walifanya hivyo kwa sababu hawakuwa na uhakika kuwa unatembea na Baba Raila Odinga lakini sasa wanajua. Pia nilizungumza naye na akaniambia wewe ni rafiki yake wa karibu na watu wa Migori pia,” Gavana Ayacko alisema.

Bw Wanjigi anatafuta kufufua azma yake ya kisiasa na amekuwa akiwasiliana na viongozi wa upinzani ili kupata mwafaka kabla ya uchaguzi wa 2027.

Kabla ya kuzuru Migori, alikutana na kinara wa ODM Raila Odinga na kumweleza kuhusu ziara yake.

Bw Wanjigi alithibitishia kwamba walikutana Malindi, ambapo walijadili hali ya sasa ya taifa na uenyekiti wa Bw Odinga wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) miongoni mwa masuala mengine.

Mkutano wa Malindi ulikuwa wa kwanza kwa Bw Wanjigi kufanya na Bw Odinga tangu wakutane kwa “mkutano wa chakula cha mchana” Januari.