Habari Mseto

Wanne waangamia kwenye ajali ya barabarani

October 13th, 2020 1 min read

NA FLORAH KOECH

Watu wanne wamefariki huku wengine wakiumia kwenye ajali ya gari kwenye barabara ya Airstrip Kabarnet Kaunti ya Baringo.

Polisi walisema kwamba ajali hiyo ilitokea wakati gari aina ya Toyota Land Cruiser Lilipoteza mwelekeo.

Mkuu wa polisi wa kaunti ya Baringo Robison Ndiwa alisema waliofariki ni watoto wa miaka  13 na watu wawili wazima.

“Abiria watatu walifariki papo kwa hapo huku mtoto wa miaka 13 akifariki kutokana na majeraha punde tu alipofikishwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Baringo ,” Bw Ndiwa aliambia Taifa Leo.

Mkuu huyo wa polisi alisema kwamba ajali zimeongezeka kwenye barabara hiyo huku akiwaomba madereva ambao hawafaamu barabara hiyo wawe makini.

Maafisa wa afya wa kaunti hiyo walisema kwamba abiria waliohumia walipata majeraha ya kichwani na kifuani.

Abiria wanne walioponea ajali hiyo walipelekwa kwenye hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi Eldoret.

Kisa hicho kimefikisha watu watano ambao wamefariki kwa ajali wiki moja iliyopita kaunti ya Baringo.

Amon Kipkirui wa miaka 27 amaarufu Rhino Kaboom alifariki baada ya pikipiki yake kugogana na gari aina ya Probox kwenye barabara ya Emining -Eldama -Ravine.

Mwili wa mwanamziki huyo ulipelekwa kwenye chumba cha maiti cha  Eldama -Ravine ,dereva wa gari hiyo  walihepa kifo bila kuumia.

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA