WANTO WARUI: Likizo ya majuma 18 kwa wanafunzi wa gredi ya 4 haifai

WANTO WARUI: Likizo ya majuma 18 kwa wanafunzi wa gredi ya 4 haifai

NA WANTO WARUI

HUKU wanafunzi wakijaribu kung’ang’ana ili warejelee hali ya kawaida ya masomo baada ya kuvurugwa na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, Wizara ya elimu tayari imetoa kalenda ya shule inayotoa mwelekeo hadi mwaka wa 2023.

Katika kalenda hiyo, wanafunzi wa Gredi ya 4 ambao iliwabidi kufungua mapema kidogo pamoja na darasa la 8 na kidato cha 4, wamepangiwa kukaa nyumbani kwa majuma kumi na manane – takriban miezi minne na nusu, katika likizo ijayo.

Hivi ni kusema kuwa baada ya wanafunzi wa Gredi ya 4 kufunga shule tarehe 19/03/2021 watakaa nyumbani hadi wafungue tarehe 26/07/2021.

Wizara ya Elimu imepanga kalenda hiyo hivyo kwa kutoa sababu kwamba wanafunzi wa Gredi ya 4 walitangulia shuleni wakati ya wenzao waliokuwa nyumbani. Aidha, inatazamiwa kuwa silabasi ya Gredi ya 4 itakuwa imekamilika kufikia Machi 19, wakati wa kufunga shule.

Jambo jingine ambalo huenda lilichangia wanafunzi hao kupangiwa hivyo ni kwa lengo la kurejelea mwaka wa masomo pamoja na wenzao hapo Julai 26, 2021 ili waingie Gredi ya 5.

Ingawa ni mpango mzuri, kuwataka wanafunzi kukaa nyumbani tena kwa miezi minne na nusu baada ya kusoma tu kwa mihula miwili mifupi ni kuwakosea.

Ni vyema ikumbukwe kuwa wanafunzi hao bado wangali na makovu ya vidonda vya Covid-19 kwa kukaa bila masomo kwa miezi tisa.Haina maana halisi kutoa sababu za kuwaweka nyumbani tena kwa muda mrefu vile. Mpango maalum ungeundwa wa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawa wanaendelea na masomo yao badala ya kulaza damu tu kule nyumbani.

Wizara

Kwa mfano, Wizara ya Elimu ingeagiza baraza la mitihani nchini, KNEC, kuandaa mafunzo na majaribio angalau ya miezi miwili kama yale waliyofanya katika Gredi ya 3 ambayo yangewaweka wanafunzi hao katika hali bora zaidi ya kujitenga kutokana na ushawishi mbaya wakiwa nyumbani.

Mpango kama huu ungewaokoa wanafunzi hawa kutoka kwenye uzembe wa kukaa tu nyumbani. Aidha, ungetatua tatizo la kuwapa wazazi mzigo mkubwa wa kuwindana na wana wao mchana ilhali mahitaji ya kuwakimu yanahitajika.

Licha ya kuwa wanafunzi wa Gredi ya 4 wamekuwa shuleni kwa mihula miwili, bado kuna kazi nyingi sana ambazo hawajaweza kuzifanya ambazo zinahusiana na masomo yao.

Kwamba ndiyo gredi inayotanguliza mfumo wa CBC, kuna kila sababu ya kuwatayarisha wanafunzi hawa vyema kabisa wasije wakatetereka.Na huu ndio ungekuwa wakati mwafaka zaidi wa kuandaa wanafunzi hawa wa Gredi ya Nne badala ya kuwaelekeza nyumbani tena kwa majuma 18 wakakae bure!

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: BBI ikipita mshahara wa wabunge ukatwe

Helikopta na magari ya kifahari viongozi wakimenyana wiki...