WANTO WARUI: Serikali ifanye ukaguzi wa kina wa majengo na miundomsingi shuleni

WANTO WARUI: Serikali ifanye ukaguzi wa kina wa majengo na miundomsingi shuleni

NA WANTO WARUI

KISA kilichotokea juma lililopita katika shule ya msingi ya Gituamba, eneo la Ruai, Nairobi kiliwaacha wazazi wengi vinywa wazi baada ya kuona mipasuko mikubwa katika kuta za baadhi ya madarasa.

Mipasuko hiyo ambayo yamkini imekuwepo madarasani humo kwa muda mrefu ilizua wasiwasi kwa wanafunzi wa shule hiyo ambao, kutokana na taarifa za wazazi wengine, walikuwa washaanza kukataa kuhudhuria mafunzo shuleni kwa sababu ya uoga wa kuangukiwa na madarasa.

Kulingana na walimu, wanafunzi walisikia mtetemeko madarasani nao wachomoka mbio kuyanusuru maisha yao.

Ilibidi walimu kuwafunzia nje kwenye jua, mavumbi na upepo mkali. Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo, mipasuko hiyo ilianza siku nyingi zilizopita ikawa inapanuka kidogo kidogo tu mpaka ilipofikia kiasi hicho.

Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo akitoa kauli yake alisema kuwa, kulikuwa na kasoro tangu mwanzo wa ujenzi wa madarasa hayo kwani kuna nguzo muhimu ambazo hazikujengwa.

Shule hii ya Gituamba ni mojawapo miongoni mwa nyingi ambazo ziko katika hali duni. Ni miaka michache tu iliyopita tuliposhuhudia vifo vya wanafunzi baada ya kuporomokewa na madarasa katika Shule ya Talent Academy, Nairobi.

Aidha tumewahi kushuhudia shule nyingi ambazo ziko katika hali mbaya zaidi. Katika baadhi yazo, majengo ya vyoo ni mabovu sana na yaliyobomokabomoka hivi kwamba, ni hatari mno kwa wanafunzi.

Vilevile, kuna baadhi ya shule ambako kuna ulegevu wa utendakazi na upuuzaji wa mambo unaoweza kusababisha maafa shuleni.

Utakuta nyaya za umeme zimeachwa kiholela, swichi zimevunjikavunjika, kwingine hakuna vifaa vya kuzima moto na kwingine kuna mashimo ambayo ni hatari kwa watoto wakicheza.

Katika baadhi ya shule, hakuna maji safi ya kunywa na hata maji taka yanayonuka hupitia ndani ya shule. Haya yote ni masuala nyeti ambayo yanafaa kuchunguzwa na kurekebishwa ili kufanikisha usalama wa wanafunzi shuleni.

  • Tags

You can share this post!

Aliyening’inia kwa ndege kushtakiwa leo Jumatatu kwa...

TAHARIRI: Serikali ije na mikakati mipya kubabili utumizi...

T L