WANTO WARUI: Serikali itoe mwelekeo kuhusu elimu ya juu ya CBC kusaidia mipangilio inayofaa

WANTO WARUI: Serikali itoe mwelekeo kuhusu elimu ya juu ya CBC kusaidia mipangilio inayofaa

Na WANTO WARUI

JUMA lililopita, Katibu Mkuu katika Wizara ya Elimu, Bi Fatuma Chege, alitoa taarifa kuhusu ni wapi ambako wanafunzi wa Gredi ya Saba watasomea ifikapo mwaka wa 2023.

Bi Chege alielezea kuwa masomo ya Gredi ya saba hadi tisa yatakuwa katika shule za sekondari wala sio katika shule za msingi kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali.

Akitoa taarifa hiyo, alisema kuwa kuna baadhi ya masomo ambayo ni muhimu sana katika kumwelekeza mwanafunzi kuchagua mwelekeo wake wa maisha hasa vipaji na ajira.

Alisema kuwa shule za msingi bado hajizaweza kuweka mikakati madhubuti ya kuweza kushughulikia masomo ya kiwango hicho.

Kwa mfano, kuna vifaa vingi vinavyohitajika ikiwemo maabara, pembejeo za Somo la Kilimo, majengo ya masomo ya Sanaa na Sayansikimu miongoni mwa vifaa vingine.

Aidha walimu wa kuwaelekeza na kuwafunza wanafunzi pamoja na mtagusano wa wanafunzi wa sekondari na wale wa shule ya msingi zitakuwa na changamoto nyingi.

Kuna uwezekano kuwa mwelekeo anaoutoa Bi Chege ndio ufaao kutayarisha wanafunzi hawa ili waweze kufikia malengo tarajiwa.

Hata hivyo, matangazo na taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na viongozi katika sekta ya Elimu zinawachanganya walimu na wazazi kila uchao.

Hapo awali, maelekezo yalieleza kuwa wanafunzi wa Gredi ya 7 hadi 9 watasomea katika shule za sekondari pamoja na zile za msingi zilizo na nafasi za kuwakimu wanafunzi.

Baadhi ya washirika wa elimu wengine wakiwa wakurugenzi wa shule za kibinafsi za msingi walikuwa washaanza matayarisho kwa ajili hiyo.

Ni vyema Wizara ya Elimu itoe mwelekeo kamili ili walimu, wazazi na wanafunzi waweze kufuatilia bila tashwishwi tele.

  • Tags

You can share this post!

Man-City wazamisha West Ham tena na kuendeleza ubabe wao...

Kibarua cha Raila waasi wakirejea ODM

T L