WANTO WARUI: Serikali iweke mipango madhubuti ya masomo ya gredi ya 7, 8, 9

WANTO WARUI: Serikali iweke mipango madhubuti ya masomo ya gredi ya 7, 8, 9

NA WANTO WARUI

JOPOKAZI lililoteuliwa na Rais William Ruto ili kuchunguza na kutoa mapendekezo yake kuhusu mtaala mpya wa elimu, CBC, limependekeza wanafunzi wanaojiunga na Gredi ya 7 waendelee kukaa katika shule za msingi ila wawe na maabara na walimu wao.

Pamoja na hayo, watahitaji pia kuwa na sare tofauti na zile za shule ya msingi, na mambo mengine kadhaa.

Ikiwa hivyo ndivyo itakavyokuwa, serikali inahitaji kuweka mipango maalum kwani kuna mambo kadhaa ambayo yanahitaji kutendwa kwa uangalifu ili kufaulisha masomo hayo.

Baadhi ya mambo hayo ni kuwepo kwa walimu waliohitimu kufunza masomo ya sekondari. Pia kutakuwa na mchanganyiko wa utendakazi miongoni mwa walimu na wafanyakazi wengine.

Walimu ambao watakuwa wakifunza sehemu ya sekondari watakuwa na shida ya mwingiliano na wale walio katika shule ya msingi. Shida nyingine kubwa ambayo itatatiza masomo ya sekondari tangulizi katika shule za msingi ni ukosefu wa walimu waliohitimu kufundisha katika ngazi hiyo.

Shule nyingi zitawatumia walimu wale wale wanaofunza shule za msingi licha ya kuwa hawajahitimu katika kazi hiyo.

Serikali inafaa kuhakikisha kuwa inatimiza ahadi yake ya kuwaajiri walimu 116,000 ilivyosema katika kampeni zake.

Walimu watakaofunza sekondari tangulizi wapewe mafunzo kikamilifu ili waweze kutimiza malengo ya masomo ya kiwango hicho.

Wizara ya elimu ikiongozwa na Waziri Ezekiel Machogu haina budi kuhakikisha kuwa walimu wa kutosha na wenye mafunzo yafaayo wameajiriwa.

Kwa upande mwingine, wadau katika sekta ya kibinafsi pia wanafaa wapewe fursa ya kutekeleza mpango huu wa sekondari za tangulizi kwani wana uwezo wa kujiandaa ipasavyo.

Tayari kuna watu binafsi ambao wamejenga shule za sekondari za chini kama ilivyokuwa imependekeza serikali ya awali ya Uhuru Kenyatta. Kwa wale ambao walikuwa washajenga sekondari hizo itakuwa ni hasara kubwa kwao. Itabidi watafute mbinu za kutumia madarasa hayo mapya.

Mradi mzima wa sekondari za chini haukufaa kuwa katika shule za msingi wala za sekondari.

Maoni ya Jopokazi huenda yalipendekeza tu pendekezo hili ili kutatua shida iliyopo kwa muda. Ukweli ni kwamba shule za sekondari za chini, Gredi ya 7,8 na 9 hazifai kuwa pamoja na shule nyinginezo zozote. Zinafaa kuwa zimejisimamisha zenyewe bila ushirika wowote wa shule za msingi au za sekondari kuu.

Kutoka na pendekezo hili la jopokazi, matatizo mengi ambayo yatatatiza masomo bado yatajitokeza. Kuna haja ya kuangalia mfumo wenyewe wa elimu kwa jicho la ndani zaidi wala si kutatua tu shida kwa muda mfupi tu.

  • Tags

You can share this post!

Kiptum azoa Sh13m baada ya kushinda Valencia Marathon

Bangi yanaswa ikisafirishwa kwa basi la Dreamline

T L