WANTO WARUI: Tutahadhari kuhusu corona Kidato cha Kwanza wakiripoti wiki hii

WANTO WARUI: Tutahadhari kuhusu corona Kidato cha Kwanza wakiripoti wiki hii

Na WANTO WARUI

Huku wanafunzi wa kidato cha kwanza wakiripoti katika shule zao mpya za sekondari hii leo, kuna uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kuingia katika baadhi ya shule kwani wanafunzi hao wamekuwa nje kwa muda mrefu sana na wamekuwa wakitangamana na watu mbalimbali mitaani.

Wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wamekuwa mapumzikoni tangu mwezi wa Machi walipokamilisha masomo yao ya msingi na kufanya mtihani wa kuwawezesha kujiunga na shule za upili.

Kutokana na ukweli kwamba muda huo ni mrefu sana na wengine wamekuwa wakitembelea jamaa zao katika maeneo tofauti tofauti humu nchini, uwezekano upo wa kuambukizana ugonjwa huu.

Pamoja na hayo, kutoka siku ya leo na wiki hii kwa ujumla, shule zote za sekondari kote nchini zitakuwa na wageni ambao ni wazazi na marafiki wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza.

Kufikia sasa, takwimu za Wizara ya afya zinasema kuwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 yameongezeka na kufikia asilimia kumi na nne huku kukiwa na wasiwasi kuwa huenda yakaendelea kuongezeka.

Hili linachangiwa zaidi na mikusanyiko ya watu katika mikutano ya siasa inayoendelea katika sehemu mbalimbali kote nchini.

Aidha, idadi kubwa ya wananchi imeanza kupuuza masharti ya Covid-19 yaliyotolewa na Wizara ya afya kama vile kunawa mikono, kutokaribiana, kuvaa barakoa na kupima joto.

Walimu wakuu wa shule zote hasa za sekondari hawana budi kukazia macho suala hili la masharti ya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 na kuhakikisha kuwa kila mgeni anayeingia shuleni ameyazingatia.

Pia ndani ya shule wanafunzi wanafaa kupimwa mara kwa mara na iwapo kuna wale watapatikana na dalili hizi basi watengwe haraka na wizara ya afya ijuzwe.

Jambo jingine ambalo ni muhimu sana ni kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anayefanya kazi shuleni amepokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid -19.

Bado serikali haijaonesha kuwajibika kwake katika suala hili shuleni. TSC pamoja na Wizara ya Elimu zinafaa kuungana pamoja na kulazimisha kila mfanya kazi wa shuleni apewe chanjo ya kujikinga na Covid -19.

Hii ni njia mojawapo ambayo inaweza kuzuia kwa asilimia kubwa sana kusambaa kwa ugonjwa huu hasa katika shule zote.

Hatari nyingine inayoweza kusambaza ugonjwa huu haraka ni kuwa dalili za Covid -19 hazionekani wazi hasa kwa vijana na watoto wa shule.

Hivi ni kusema kuwa kila shule ina jukumu la kupima wanafunzi wakemara kwa mara wanapokuwa shuleni ili kubaini usalama wao. Aidha kipindi hiki cha baridi kinaweza kuchangia sana maambukizi kwani maradhi mengi ya baridi yanaibuka sasa.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Wapigakura wajifunze kutoka ahadi feki 2017

Kalonzo amrai Shahbal arejee chamani Wiper