WANTO WARUI: Wanafunzi walio katika shule za maeneo hatari walindwe

WANTO WARUI: Wanafunzi walio katika shule za maeneo hatari walindwe

NA WANTO WARUI

WANAFUNZI wengi katika taifa hili wamekuwa wakiathirika zaidi kimasomo kutokana na ukosefu wa kiusalama katika maeneo kadha wa kadha nchini. Mojawapo ya hali hizi ni eneo linaloathirika sasa la Ol Moron katika kaunti ya Laikipia.

Wanafunzi wengi ambao wanasomea Ol Moron kwa sasa hawajui watarejelea masomo yao lini baada ya kufurushwa makwao na waasi ambao waliwachomea shule.

Kwa sasa wanafunzi hao pamoja na jamaa zao wamehama eneo hilo na hawana mahali maalum ambapo wanaweza kuishi ili kuendeleza masomo yao.

Familia nyingi ambazo zimefurushwa hazina chakula, mavazi wala malazi kutokana na kutekwa kwa mifugo yao na hata kuchomewa nyumba na majambazi hao sugu.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi wa Aprili, mwaka huu wanafuzi wengine wengi walijipata wakipoteza masomo yao baada ya kufurushwa kutoka maeneo waliyoita nyumbani huko Makima, Mbeere Kusini.

Katika tukio hilo, familia za wanafunzi hao zilijipata zikihamishwa kwa nguvu bila kujali wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo yao.

Hali hii ilisababisha usumbufu na ukosefu wa amani na utulivu kwa wanafunzi, jambo ambalo linaweza kuwaathiri katika maisha yao ya usoni.

Aidha, hali ya ukosefu wa usalama ingali inaendelea katika kaunti ya Baringo. Kuna wanafunzi wengi ambao pia wamehama shule au kutoka wanakoishi kwa sababu za ukosefu wa amani.

Pia kuna wale ambao wamehama kutokana na hali mbaya ya mjazo wa ziwa ambao umekuwa ukitishia maisha ya familia nyingi katika kaunti ya Baringo. Vivyo hivyo tuliweza kuona wananchi wengine wakihama kule Naivasha karibu na kingo za ziwa baada ya maisha yao kutishiwa na maji.

Kaunti ya Narok nayo huwa na visa vya mara kwa mara vya uvamizi ambavyo huathiri sana jamii zinazoishi huko. Kuna maeneo mengine yanayokosa utulivu kama vile kule Tana River.

Misukosuko hii yote inawaacha maelfu ya wanafunzi wakihangaika kwa kupoteza masomo huku wengine wakiacha shule kabisa au hata kuuawa katika vurugu hizo.

Taifa la Kenya sasa linajivunia miaka 58 tangu kujinyakulia uhuru na ni makosa makubwa ikiwa bado kuna wanafunzi wanaokosa masomo kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Serikali inafaa kuwa ange na kuweka mikakati imara kabisa ambayo itazuia kuzuka kwa vurugu kama zile tunazoshuhudia kule Laikipia.

Magenge ya wahalifu yaangamizwe na kama kuna wachochezi watiwe mbaroni na kukabiliana na mkono wa sheria. Maeneo yote ambayo yanatishiwa na hali za ukosefu wa usalama yanafaa kulindwa kwa ajili ya jamaa wanaoishi huko na zaidi kuwawezesha watoto walio katika sehemu hizo kupata elimu ili wajikomboe kutoka katika minyororo ya umaskini.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Siasa zimesaidia wafisadi kuendelea...

TAHARIRI: Makanisa mengine nao waige mfano kanisa la ACK