WANTO WARUI: Wazazi washirikishwe katika uchaguzi wa shule za upili za daraja ya chini

WANTO WARUI: Wazazi washirikishwe katika uchaguzi wa shule za upili za daraja ya chini

NA WANTO WARUI

HUKU uchaguzi wa shule za sekondari za daraja la chini ukianzishwa leo na Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na KNEC, hapana shaka wanafunzi wa Gredi ya Sita hawataweza kufanya maamuzi yafaayo katika uchaguzi huo.

Ni vyema walimu wawashirikishe wazazi au walezi wa wanafunzi hao ili wawasaidie katika zoezi hilo muhimu.

Tumeshuhudia wanafunzi wa Darasa la Nane wakichagua shule peke yao bila usaidizi wa wazazi na hatimaye matokeo yakawa kuchagua shule za kifahari au zilizo mbali sana na kwao jambo ambalo liliwaharibia nafasi za kujiunga na shule za viwango vyao.

Wanafunzi wa Gredi ya Sita ni wadogo mno wakilinganishwa na wale wa Darasa la Nane.

Hawawezi kutoa maamuzi yafaayo kabisa kwani kwao hawaelewi shule hizo kamwe.

Licha ya hayo, ni muhimu sana kutambua umri wa wanafunzi hawa ni mdogo na hawataweza kujiunga na shule za sekondari za malazi. Hawajakomaa kiasi cha kuweza kujifulia nguo, kujiwekea vitu vyao vizuri kwa mpango ufaao au hata kukaa mbali na wazazi wao.

Kwa hivyo, ni vyema wazazi wawaongoze kikamilifu ili waweze kuchagua shule zilizo karibu na mahali wanapoishi na ambapo hawatachoka sana wakitembea.

Kwa wale wanaoishi mijini, ni vizuri wasichague shule ambazo zinahitaji usafiri wa zaidi ya gari moja kwani mwanafunzi atatatizika sana.

Wizara ya Elimu izingatie kwa makini sana uadilifu wakati itakakuwa ikiwateulia wanafunzi hao shule.

Kipindi cha nyuma, licha ya wanafunzi kuchagua shule walizopendelea, serikali ilikuwa ikiwateulia shule zilizo mbali sana na kwao nyingine hata zikiwa ni za kutwa.

Wazazi na walimu walipolalamikia jambo hilo Wizara ya Elimu ilijitetea kwa kusema kuwa ni uchaguzi mbaya wa shule ama ni kompyuta iliyofanya kazi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

ODM matumaini tele kuhifadhi ugavana Mombasa

Mshindi wa kiti cha ubunge Malindi atuliza hofu baada ya...

T L