Habari MsetoSiasa

Wanyakuzi wa Mau kushtakiwa, Kamishna asema

September 22nd, 2019 2 min read

KEN OPALA na JULIUS SIGEI

SERIKALI sasa iko tayari kushtaki watu wenye ushawishi mkubwa nchini ambao walihusika katika unyakuzi wa sehemu kubwa ya ardhi ya Msitu wa Mau yenye ukubwa wa hekta 46,000.

Kamishna wa Kanda ya Rift Valley George Natembeya anasema serikali imekusanya stakabadhi zote husika na kuiwezesha kufunguliwa mashtaka watu hao kwa kuharibu msitu huo ambao ni mojawapo ya chemchemi kubwa za maji nchini.

Miongoni mwa wale ambao watashtakiwa ni wanasiasa wakuu na waliokuwa maafisa wa Wizara ya Ardhi Narok na Nairobi unyakuzi huo ulipotekelezwa. Wengine ni maafisa wa lililokuwa baraza la mji wa Narok na viongozi wa ranchi mbalimbali zilizomiliki ardhi karibu na msitu huo.

“Maafisa wote wa serikali waliohusika tayari wameandikisha taarifa. Na waliofariki, tumeenda katika makaburi yao kudhibitisha kuwa kweli wameaga dunia. Tuko na stakabadhi zao za kifo,” Bw Natembeya akaambia Taifa Leo katika mahojiano ya kipekee.

Hatua hiyo, ya kuwashtaki wahusika wa unyakuzi wa ardhi na uharibifu wa Msitu wa Mau, inajiri miongo mitatu baada ya juhudi za serikali kuwaadhibu watu hao kucheleweshwa kutokana na mivutano ya kisiasa na uzembe wa maafisa husika.

“Tumewasilisha faili zao kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji hivi karibuni wanakamatwa na kushtakiwa,” Bw Natembeya akasema.

Kushtakiwa kwa watu hao kutaendeshwa sambamba na mchakato wa kufurushwa kwa zaidi ya familia 6,000 za walowezi kutoka eneo la msitu huo lililoko kaunti ya Narok, maarufu kama Maasai Mau.

Ilani ya siku 60 iliyotolewa na serikali kwa wao kuondoka inakamilika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

Sehemu ya msitu huo ambayo imenyakuliwa ina ukubwa wa hekta 17,101 kati ya eneo asilia la ukubwa wa hekta 45,743.8. Hii na kando na eneo la ukubwa wa hekta 32,000 ambayo ni sehemu iliyotengwa kupanda miti kupanua msitu huo.

“Kulikuwa na ilani iliyowekwa mnamo 2009 dhidi ya watu kuingiliwa ardhi ya msitu wa Mau lakini unyakuzi uliendelea,” akasema Bw Natembeya.

Watu wengine wanaomulikwa ni masoroveya, maafisa wa wizara za ardhi na misitu na viongozi wa ranchi tano zilizomiliki ardhi karibu na msitu huo.

Viongozi wa ranchi hizo- Reiyo, Enkaroni, Sisiyan, Enaikishomi na Enoosokon- walitumia vibaya amri ya Rais wa zamani Daniel Moi mnamo miaka ya 1990 kwa wagawanya ardhi zao. Lakini katika kufanya hivyo, walivamia ardhi ya karibu ya Msitu wa Maasai Mau.

Baada ya kuvuka mipaka yao, wakuu wa ranchi hizo walishirikiana na masoroveya, maafisa wa lililokuwa wa baraza la mji wa Narok, maafisa wa wizara za Ardhi na Misitu pamoja na maafisa wengine waliokuwa ushawishi serikalini.

Maafisa wanaolengwa katika sakata hiyo ni masorovya Jackto Mogaka, George Gaya, Sila Muketha, Fancis Kipngetich na Joseph Mukhole. Wengine ni wasajili wa ardhi John Chepkirui (marehemu), A.S Bamosa naJoseph Onyambu.

Maafisa wa ranchi walioshiriki unyakuzi huo ni pamoja na Napatau ole Kana na Rukuti Ole Konata na Sanja ole Sankei (ranchi ya Sisiyan ).

Maafisa wengine ni; Sampele Ole Maleto, Fredrick Cheres na Benson Kori (Ranchi ya Reiyo), Oloosuya Ole Tiyo, Juma Ole Kimanyim and Lemein Ole Kiputa (Ranchi ya Enoosokon ), na Mbw David Lekuta ole Sulunye, Mr Stanley Naiyeya Sirma na William ole Sirma (wa ranchi ya Enaikishomi).