Habari

Wanyama akutana na DP Ruto makala ya pili ya Wanyama Roya Charity Cup yakinukia

July 12th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa timu ya soka ya Kenya ya wanaume, Victor Mugubi Wanyama alitembelea Dkt William Ruto katika afisi yake ya Karen hapo Julai 11 katika kile Naibu huyo wa Rais alisema ni kuunga mkono juhudi za ukuzaji wa talanta ya kimichezo.

“Tunaunga mkono juhudi za kutafuta talanta za michezo na kukuza chipukizi ili waweze kuzitumia kujiendeleza kimaisha pamoja na kutafutia riziki kama wachezaji wa kulipwa.

“Kupatia nguvu sekta ya michezo kupitia ukusanyaji wa raslimali za kutosha na kuunda miundombinu ni kitu muhimu katika kuhakikisha vijana wanafanikiwa michezoni na kuisha maisha mema,” Naibu Rais alichapisha ujumbe huo kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kukutana na kiungo huyo wa Tottenham Hotspur pamoja na ndugu zake McDonald Mariga Wanyama na Thomas Khumba Wanyama.

Naibu Rais William Ruto azungumza wakati ambapo alitembelewa na Victor Wanyama. Picha/ Hisani

Itakumbukwa Dkt Ruto ni mmoja wa wageni mashuhuri waliohudhuria uzinduzi wa mashindano ya Roya Charity Cup mwaka 2018.

Mashindano haya ya muondoano yalizinduliwa jijini Nairobi mnamo Juni 2018 na Wanyama na Mariga yakilenga kukuza talanta hasa kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 16.

Ushindi wa Dandora Youngsters

Makala hayo ya kwanza yalifanyika katika siku mbili (Juni 30 na Julai 1) katika Shule ya Upili ya St Marys kwenye barabara ya James Gichuru jijini Nairobi.

Dandora Youngsters iliibuka mshindi baada ya kulipua Mainstream FC kutoka mtaani Kawangware 3-0.

Makala ya pili yamepangiwa kufanyika katika kaunti zote kabla ya jiji la Nairobi kuandaa fainali. Tarehe bado hazijatangazwa.

Mwaka 2018, timu zilizokamilisha katika nafasi nne za kwanza Dandora Youngsters, Mainstream, Green Santos na Young Talent zilitengewa zawadi ya Sh500,000, Sh300,000, Sh100,000 na Sh50,000, mtawalia.