Michezo

Wanyama alishwe benchi, mashabiki washauri

June 24th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Harambee Stars wanataka nahodha Victor Wanyama atupwe kwenye benchi Kenya itakapokutana na Taifa Stars ya Tanzania katika mechi yake ya pili ya Kombe la Afrika (AFCON) jijini Cairo nchini Misri hapo Juni 27, 2019.

Walikerwa na mchango mdogo sana wa kiungo huyu katika mechi dhidi ya Algeria ambayo mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) walikanyagwa 2-0 kupitia mabao ya Baghdad Bounedjah na Riyad Mahrez yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza.

Baada ya mchuano huo, Wakenya walimlaumu Wanyama, 27. Shabiki Lawi Ragwanda alisema, “Wanyama anasifiwa bure tu; alifanikiwa tu kusababisha ikabu.”

“Sioni kwa nini asitiwe kwenye benchi katika mechi ijayo. Hakuwa na ushawishi hata kidogo (dhidi ya Algeria),” alilia Otieno Dave.

Naye Wish Kiptoo alisema, “Si eti nachukia Wanyama, lakini nahisi hakuchangia kitu muhimu kusaidia timu. Matarajio yangu yalikuwa kuona akitoa mchango mkubwa, lakini nimebaki na masikitiko tu.”

Kongo Eldwin Ongeto alisema, “Wanyama ana kasi ya konokono ambayo haiwezi kuwa motisha kwa wengine.”

Mchezo wa Wanyama katika mchuano huo pamoja na AFCON ulitarajiwa kushawishi waajiri wake Tottenham Hotspur kubadili mawazo ya kutaka kumuuza, lakini baada ya kuonyesha kiwango cha chini cha mchezo huenda klabu hiyo kutoka jijini London nchini Uingereza ikawa imeridhika inafanya tendo la busara kumuondoa katika kikosi chake.

Wanyama amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu msimu 2017-2018, huku akifanikiwa kusakata mechi 13 pekee ligini msimu 2018-2019 ambazo tena hakuhusishwa dakika zote 90.