Wanyama aongoza klabu kutwaa ubingwa Canada

Wanyama aongoza klabu kutwaa ubingwa Canada

Na JOHN ASHIHUNDU

Aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama ameweka historia nchini Canada baada ya kusaidia klabu yake ya CF Monteal Impact kuhifadhi ubingwa wa Kombe la Washindi nchini Canada (maarufu kama Canadian Championship) baada ya kuichapa Toronto 1-0 kwenye fainali, Jumapili.

Bao hilo muhimu lililoiwezesha Montreal kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa kwa mataifa ya CONCACAF lilifungwa na Romell Quioto dakika ya 72 ugani Stade Saputo.Mbali na tiketi ya kufuzu kwa michuano hiyo ya bara, kadhalika mabingwa hao walipokea Sh8.5 milioni baada ya pambano hilo ambalo Wanyama alicheza mechi yote.

Montreal ilitinga fainali baada ya kuibwaga HFX Wanderers 3-1 katika hatua ya robo-fainali na baadaye Forge 8-7 kwenye nusu-fainali kupitia kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi kumalizika kwa 0-0 katika muda wa kawaida.Toronto walifuzu baada ya kuibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya York United katika robo-fainali kabla ya kuinyamazisha Pacific FC 2-1 katika nusu-fainali.

Montreal wametwaa ubingwa wa mashindano hayo mara tano tangu 2008, huku Toronto wakijivunia ushindi mara saba.Michuano ya Canadian Championship inahusisha wachezaji wa klabu zinazocheza soka ya kulipwa nchini humo ambapo washindi wanapata tiketi ya kushiriki katika michuano ya Ligi ya Kombe la Washindi kwa mataifa ya CONCACAF.Timu zingine zilizofuzu kwa michauno ya Concacaf ni New England Revolution, Colorado Rapits na Seattle Sounders.

You can share this post!

Kipusa Mbuche kusajiliwa na TSC Queens ya Tanzania

Man Utd leo kwenye kibarua kingine Uefa

T L