Michezo

Wanyama asema hana pupa ya kujiunga na Club Brugge

August 27th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Victor Wanyama hana haraka ya kujiunga na Club Brugge hadi pale atakuwa na uhakika klabu hiyo ya Ubelgiji itashiriki mechi za makundi za Klabu Bingwa Ulaya, ripoti nchini Uingereza zinadai.

Brugge itaalika LASK Linz kutoka Austria katika mechi ya marudiano ya kuingia mechi za makundi za Klabu Bingwa hapo kesho. Inaongoza Linz 1-0 baada ya kuishinda japo pembamba katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Agosti 20.

Nahodha huyu wa Harambee Stars ameteremka katika orodha ya viungo wa Spurs, huku kocha kutoka Argentina, Mauricio Pochettino akikiri kuwa amemshiba mchezaji huyu wa zamani wa Nairobi City Stars, AFC Leopards, Helsingborg (Uswidi), Beerschot (Ubelgiji), Celtic (Scotland) na Southampton (Uingereza) kutokana na kutotegemewa na timu hiyo kutoka jijini London.

Wanyama alihusishwa na karibu klabu tano nchini Uingereza zikiwemo Bournemouth na West Ham, lakini hakuna iliyomnunua kufikia siku ya mwisho ya kipindi kirefu cha uhamisho mnamo Agosti 9.

Uhamisho hadi Brugge umezungumziwa kwa muda sasa, huku ripoti nchini Ufaransa zikidai kuwa klabu hiyo iliambiwa bei yake ni Sh1.7 bilioni.

Wanyama alianzia soka yake ya malipo nchini Ubelgiji mwaka 2008 katika klabu ya Beerschot, ambayo ilivunjika mwisho wa msimu 2012-2013 kutokana na matatizo ya kifedha.

Ripoti nchini Uingereza zinaonya kuwa uhamisho wa Wanyama hadi Brugge huenda ukagonga mwamba ikiwa klabu hiyo haitaingia mechi za makundi za Klabu Bingwa.

Licha ya kuongoza Linz kupitia bao lililofungwa kwa njia ya penalti na Hans Vanaken nchini Austria na pia kuwa nyumbani, nafasi ya Brugge katika Klabu Bingwa si salama.

Linz ilibandua miamba wa Uswizi Basel kwa jumla ya mabao 5-2 wiki mbili zilizopita kwa hivyo uwezo wake wa kusababishia Brugge madhara hauwezi kupuuzwa.

Fursa ya kusakata katika Klabu Bingwa, ripoti zinasema, itakuwa kivutio kikubwa kwa Wanyama, ambaye hakuchezea Spurs katika mechi tano za kujiandaa kwa msimu mpya akiuguza jeraha na pia amekosa mechi tatu za kwanza za ligi.

Alikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba dhidi ya Aston Villa mnamo Agosti 10, lakini hakutumiwa kabla ya kuondolewa kabisa kikosini. Pochettino alinukuliwa juma lililopita akisema Tottenham si shirika la kutoa misaada kwa wachezaji waliopiga hatua nyuma kama Wanyama.

Wanyama, ambaye miamba wa Uturuki Galatasaray na Fenerbahce pia walihusishwa naye katika kipindi hiki cha uhamisho, alichezea Spurs mara ya mwisho dhidi ya Everton mnamo Mei 12.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu ilitamatika 2-2 uwanjani Tottenham. Hakutumiwa na Spurs katika fainali ya Klabu Bingwa mnamo Juni 1, ingawa alikuwa kitini ikichapwa 2-0 na Liverpool.

Inasemekana mara tu mechi ya marudiano kati ya Brugge na Linz kusakatwa, Wanyama atafanya uamuzi wake wa mwisho.