Michezo

Wanyama ataka FKF ishauriane na FIFA kuhusu Amrouche

April 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa Harambee Stars na kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, Victor Wanyama, amelisihi Shirikisho la Soka la Nchini (FKF) kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake kuhakikisha kwamba Kenya inashiriki mechi zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

“Nahisi kwamba tuna nafasi kubwa ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia hasa ikizingatiwa wapinzani tuliopangwa nao kundini. Itakuwa aibu kwa FKF kutamauka na kuzima ndoto za wanasoka wengi ambao pengine milango ya heri kitaaluma ingewafungukia kwa kushiriki mechi hizo,” akatanguliza Wanyama, 28.

“Itakuwa aibu sana kwa Kenya kukosa fursa hii adhimu. Ningependa FKF ijitahidi kadri na uwezo na kunyosha mambo. Japo makataa yamepita, itakuwa vyema kushauriana na FIFA zaidi ili muda huo uongezwe. Sidhani watakosa kuelewa hasa ikizingatiwa ukubwa wa changamoto zinazoshuhudiwa kwa sasa katika ulingo wa michezo dunia kote,” akasema Wanyama ambaye kwa sasa anachezea Motreal Impact ya Canada.

Chini ya kocha Francis Kimanzi, Harambee Stars kwa sasa wanakabiliwa na hatari ya kutupwa nje ya kampeni hizo baada ya kushindwa kumfidia kocha Adel Amrouche Sh109 milioni kufikia mwisho wa Aprili 23, 2020 jinsi ilivyoagizwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

FKF iliamrishwa kumlipa Amrouche kiasi hicho cha fedha baada ya kutimuliwa kwake mnamo Agosti 2014 kutokana na msururu wa matokeo duni. Ingawa hivyo, namna ambavyo mkufunzi huyo raia wa Algeria na Ubelgiji alivyotimuliwa ilikuwa kinyume na masharti ya mkataba kati yake na FKF.

Kenya imetiwa katika Kundi E kwa pamoja na Uganda, Mali na Rwanda katika kampeni za kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar.

Siku moja kabla ya makataa yaliyotolewa na FIFA, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF alisisitiza kwamba juhudi zao zote za kutafuta fedha za kumlipa Amrouche ziligonga ukuta na akataka Kenya kuwa tayari kwa adhabu kali ya FIFA ikiwemo kukosa gozi la kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

“Tumetafuta mbinu zote za kupata fedha hizo bila mafanikio. Tumeandikia FIFA ili itupatie muda zaidi wa kutafuta fedha hizo lakini sidhani kama watasikia kilio chetu. Tumejaribu pia kuhusisha serikali lakini kwa sasa inaelekeza juhudi zote katika vita vya kukabiliana na janga la corona,” akatanguliza Mwendwa.

“Hakuna lolote ambalo tunaweza kufanya kwa sababu hatuna fedha zenyewe. Tunasalia sasa kusubiri maamuzi ya mwisho ya FIFA. Iwapo watatupiga marufuku ya kushiriki mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022, basi ni sawa. Haitakuwa mwisho wa dunia au maisha. Tutasubiri wakati mwingine, labda 2026,” akaongeza Mwendwa.

Kwa upande wake, Mwendwa alidokeza kwamba marufuku ya FIFA itakuwa fursa nyingine kwa Kenya kumakinikia mapambano mengine badala yay ale ya kutafuta tiketi ya kuelekea Qatar.

Tuna mashindano mengi zaidi ya kushiriki mbele yetu. Mbani na Kombe la Afrika (AFCON) na CHAN, tuna mapambano ya haiba ambayo Harambee Starlets na chipukizi wetu wa vikosi vya U-17, U-20 na U-23 watashiriki katika kipindi hicho hicho cha kuandaliwa kwa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Hivyo, sioni jambo hili likiwa pigo kubwa,” akasisitiza.

FIFA iliwahi kuwapiga Zimbabwe marufuku ya kushiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi kwa kosa la kukiuka masharti ya kandarasi na kumnyima haki kocha mzawa wa Brazil, Jose Claudinei ‘Valinhos’ Georgino walipompiga kalamu mnamo Machi 2015.

Zaidi ya kutozwa faini, au (na) kupigwa marufuku, FIFA huenda ikaamua kuelekeza fedha za maendeleo ya soka ambazo Kenya hupokezwa kila mwaka kumlipa Amrouche huku FKF ikichukuliwa hatua kali za kisheria.