Michezo

Wanyama kurejea uwanjani

September 21st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa timu ya taifa ya Kenya, Victor Wanyama anatarajiwa kurejea uwanjani timu yake ya Montreal Impact ikichuana na Philadelphia Union kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) hapo Septemba 21. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 amecheza dakika zote 90 katika mechi 11 tangu awasili Montreal kutoka Tottenham Hotspur nchini Uingereza mnamo Machi 3, 2020.

Montreal ya kocha Thierry Henery inashikilia nafasi ya sita kwa alama 16 baada ya kusakata mechi 11 kwenye ukanda wa Mashariki. Philadelphia iko alama tano mbele katika nafasi ya nne.

Kwingineko, Barnsley iliyoajiri beki Clarke Oduor ilionyeshwa kadi mbili nyekundu kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uingereza ikipoteza 2-0 ugenini dhidi ya Reading uwanjani Madejski, Jumamosi. Beki Oduor hakushiriki mchuano huo ambao mabeki Mads Juel Andersen na Michal Helik walilishwa kadi nyekundu. Anauguza jeraha.

Katika Ligi Kuu ya Misri, Tanta ambayo imeajiri mshambuliaji John Avire ilikabwa 0-0 dhidi ya Masr anayochezea Cliff Nyakeya uwanjani Tanta mnamo Jumamosi usiku.

Nyakeya alikuwa kitini katika mchuano huo ambao Tanta ilikamilisha wachezaji 10 baada ya mshambuliaji Walid Adel kuonyeshwa kadi nyekundu. Avire hakuwa katika kikosi cha Tanta.

Nayo Cercle Brugge anayochezea Johana Omolo itajibwaga uwanjani dhidi ya St Truiden hapo Septemba 21. Cercle iko katika nafasi ya 11 kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa alama sita. Imecheza mechi sita kwenye ligi hiyo ya timu 18 inayoongozwa na Charleroi.