Michezo

Wanyama, Olunga kupiga jeki kikosi cha Stars Misri

November 13th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUNDI la mwisho la wachezaji wa Harambee Stars wanaosakata kabumbu ya kulipwa ughaibuni, linatarajiwa kuwasili leo nchini Misri ili kuungana na wenzao, kwa mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Fainali hizo zitaandaliwa nchini Cameroon mwaka 2021.

Stars watakabiliana na Misri kesho Alhamisi katika mechi ya ufunguzi wa Kundi G. Chini ya kocha Francis Kimanzi, Stars watashuka ugani Borg El Arab jijini Alexandria kuvaana na Misri, ambao walikuwa wenyeji wa makala yaliyopita ya AFCON, ambayo ubingwa wake ulitwaliwa na Desert Foxes ya Algeria.

Kundi la kwanza la masogora wa Stars liliondoka jijini Nairobi Jumapili.

Baada ya kukamilisha kibarua hicho kigumu dhidi ya Misri, ambao ni bingwa mara saba wa AFCON, Haarambee watakuwa wenyeji wa Togo katika mchuano wa pili uwanjani MISC Kasarani, Nairobi. Mchuano huo utachezwa Novemba 18.

Togo na Comoros ambao ni wapinzani wengine wa Kenya na Misri katika Kundi G, wameratibiwa kuvaana jijini Lome siku ya Alhamisi wiki hii.

Timu ya Kenya iliyotua nchini Misri Jumatatu ilijumuisha wengi wa wachezaji wanaotandaza soka yao katika ligi za humu nchini.

Kipa Patrick Matasi anayecheza soka ya kulipwa nchini Ethiopia pamoja na mabeki Joseph Okumu na Eric ‘Marcelo’ Ouma kutoka nchini Uswidi, ndio walisafiri na kundi la Stars lililoondoka Nairobi.

Harun Shakava wa Nkana FC nchini Zambia, Michael Olunga wa Kashiwa Reysol kutoka Japan, Ayub Timbe wa Beijing Renhe FC nchini Uchina, na nahodha Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur nchini Uingereza, ni kati ya wachezaji wa mwisho wanaotazamiwa kutua Misri hii leo Jumatano.

Ubora wa Misri

Misri watajibwaga ugani wakipigiwa upatu wa kuvuna ushindi kwa wepesi, ikizingatiwa ubora wa rekodi yao dhidi ya Stars.

Kenya haijawahi kusajili ushindi wowote dhidi ya timu hiyo katika jumla ya mechi 15 zilizopita. Ina maana kwamba masogora wa Kimanzi watakuwa wakitafuta ushindi wao wa kwanza dhidi ya Pharaohs katika jaribio la 16. Kati ya michuano sita ya awali ya kimataifa, Stars imesajili ushindi mara moja pekee, kwenye mechi ya AFCON ilipopepeta majirani Tanzania 3-2 nchini Misri.

Stars walicharazwa 3-0 na Senegal katika mechi ya mwisho ya makundi katika fainali hizo za Julai 1, 2019. Waliambulia sare tasa kabla ya kupigwa 4-1 na Tanzania katika mechi za kufuzu kwa fainali za CHAN 2020, kabla kukabwa na Uganda 1-1 na kisha kupoteza 1-0 dhidi ya Msumbiji katika mchuano uliopita wa kirafiki.

Stars wanafungua kampeni ya kufuzu kwa AFCON 2021 wakati ambapo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), linakabiliwa na sakata ya kutumia vibaya Sh244 milioni ilizopewa na serikali kabla ya makala yaliyopita ya AFCON 2019 nchini Misri.