Michezo

Wanyama, Olunga wawasili kwa mechi dhidi ya Msumbiji

October 10th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA na kiungo wa Harambee Stars, Victor Wanyama na wenzake Michael Olunga na Jesse Were wamekuwa wachezaji wa hivi karibuni zaidi kuripoti kambini kwa minajili ya mchuano wa kirafiki utakaokutanisha Kenya na Msumbiji wikendi hii uwanjani MISC Kasarani, Nairobi.

Stars watapania kutumia mchuano huo wa Jumapili kujiandaa kwa mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Misri na Togo mwezi Novemba.

Wanyama ambaye kwa sasa huchezea Tottenham Hotspur nchini Uingereza, alivalia jezi za Stars kwa mara ya mwisho mnamo Juni 2019 alipokuwa sehemu ya kikosi kilichonogesha kampeni za AFCON 2019.

Sogora huyu mwenye umri wa miaka 28 alisalia nje ya kikosi cha Stars kilichovaana na Uganda Cranes katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha jijini Nairobi mwezi uliopita.

Kiini cha Wanyama kutounga kikosi hicho cha Stars wakati huo ni wingi wa tetesi zilizokuwa zikimhusisha na uwezekano wa kubanduka Tottenham na kuingia katika sajili rasmi ya Club Brugge, Ubelgiji.

Mechi dhidi ya Msumbiji itatoa jukwaa mwafaka zaidi kwa Wanyama kuyafufua makali yake baada ya kutokuwa sehemu kubwa ya mipango ya kocha Mauricio Pochettino kambini mwa Tottenham msimu huu. Hadi kufikia sasa, Wanyama amewajibishwa na Tottenham kwa kipindi cha dakika 24 pekee katika jumla ya mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Were kushirikiana na Olunga

Were ambaye ni mvamizi matata wa Zesco United nchini Zambia atashirikiana na Olunga kuongoza safu ya mbele ya Stars ambao kwa sasa wananolewa na mkufunzi Francis Kimanzi.

Kiungo Anthony ‘Teddy’ Akumu alitarajiwa kuwasili humu nchini hapo jana usiku. Yusuf Mainge na Eric Ouma wanaopiga soka ya kulipwa nchini Slovakia na Uswidi mtawalia waliingia humu mwanzoni mwa wiki hii.

Zaidi ya Masoud Juma na Ayub Timbe, nyota mwingine atakayekosa mchuano huo ni Johnstone Omurwa wa Wazito FC ambaye kwa sasa anauguza jeraha. Ili kulijaza pengo lake, kocha Kimanzi amemwita kambini Bernard Ochieng ambaye pia ni sogora wa Wazito.

Nafasi ya Masoud na Timbe wanaosakata soka ya kulipwa nchini Algeria na Ubelgiji mtawalia, imejazwa na Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars.