Dondoo

Wanyimwa mlo kwa kusengenya bi harusi

November 4th, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

KAYOLE, NAIROBI

AKINA mama waliohudhuria harusi ya mtaani walipata aibu ya mwaka waliponyimwa mlo.

Watano hao walikuwa majirani wa Bi harusi lakini hawakuwa wamealikwa harusini, jambo lililomfanya bawabu kuwazuia kuingia ukumbini.

Kulingana na mdokezi wetu, inasemekana wanawake hao hawakuwa na uhusiano mzuri na kidosho, aliyewalaumu kwa kumsengenya ovyoovyo eti alichelewa kuolewa licha ya mshahara mnono anaopokea.

“Ingawa walikuwa wakishiriki kanisa moja akina mama hao walizoea kumharibia jina mtaani, wakidai alishindwa kuolewa licha ya kuwa na kipato kikubwa,” alisema mdokezi.

Kidosho aliposikia umbea wa akina mama hao alifyata ulimi, na akaamua kutowaalika kwenye harusi yake.

Siku ya harusi wanawake hao walipanga kuhudhuria sherehe ya kanisani na baadaye kwa hafla ya mapochopocho.

Hata hivyo, mipango yao haikufanikiwa kwani Bi harusi alikuwa ameshachapisha kadi za mwaliko, akawapa aliowathamini lakini akawaacha nje majirani hao wapenda umbea.

Baada ya kuunganishwa kanisani wageni walielekea katika ukumbi uliokuwa umetengwa kwa mlo na kunengua densi.

Akina mama hao walisalia kula kwa macho tu baada ya kuzuiwa kuingia ndani ukumbini.

“Walijaribu kuzua fujo wakidai eti ni majirani wa karibu wa Bi harusi na hawafai kufungiwa nje. Lakini walinzi walisisitiza kuwa na maagizo kutoka kwa mwanadada huyo, kwamba asiruhusu ndani wale wasiokuwa na kadi ya mwaliko,” alieleza mdokezi.

Inasemekana walimpigia simu mama ya Bi harusi kujaribu kujitetea lakini hapo pia waligonga mwamba. Mama huyo hakusita kuwalabua kwa kuwaakmbia ukweli.

“Masengenyo yenu eti asingepata mume ndiyo yalifanya awanyime kadi za mwaliko. Ashapata mume, endeleeni kuongea. Tafuteni mengine ya kusema sasa,” mama ya kidosho aliwasuta na kuwaamuru waondoke.