Makala

Waoga wa maji hawawezani na raha za kisiwa cha Lamu

April 24th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

IKIWA wewe ni mzoefu wa mazingira ya kawaida, hasa nchi kavu, na iwapo unaogopa kujaribu mandhari mapya kama yale ya bahari na majimaji, basi usifike Lamu kwani huwezani.

Lamu ni kaunti iliyogawanywa vipandevipande na Bahari Hindi.

Vipande hivyo vinatambulika kama visiwa.

Eneo hilo lina zaidi ya visiwa 35 ambavyo kila kimoja hupatikana kilomita kadhaa kutoka kwa kwingine.

Baadhi ya visiwa hivyo ni Lamu Mjini, Shela, Manda na Pate.

Pia kuna Faza, Kizingitini na Ndau ilhali vingine vikiwa Mkokoni, Kiwayu, Kiunga nakadhalika.

Kwa wanaohitajika kuvifikia visiwa hivyo lazima wasafiri kuivuka Bahari Hindi kwa kutumia boti, mashua au jahazi.

Ikumbukwe kuwa Lamu ni miongoni mwa baadhi ya kaunti za Pwani zinazopendwa na watalii wengi, ikiwemo wale wa ndani kwa ndani na kimataifa.

Hii inatokana na kuwepo kwa maeneo sufufu ya kujivinjari na kujionea mazingira yenye kuuburudisha moyo.

Maeneo hayo ni vivutio vikuu vya watalii na wageni.

Lamu pia inatambulika kwa kuwa na makavazi na turathi za aina yake ambazo pia ni vivutio vya watalii.

Hii ni wazi kuwa kwa anayezuru eneo hilo mwisho wa siku huishia kutoka akiwa na ukwasi wa historia ambayo huwezi kuipata mahali kwingine kokote ulimwenguni.

Licha ya Lamu kudhihirisha kuwa mama au baba lao katika masuala ya kujipa hepi, lazima watu wafahamu kuwa kula au kuifurahia raha halisi ya kisiwa au visiwa vya Lamu ni kuondoa woga.

Hapa, mja anapaswa kuupiga teke moyo hafifu na badala yake kuuvaa moyo wa simba ili kumwezesha kula hepi asilia au ya uhakika kwenye visiwa vya Lamu.

Hili linatokana na kwamba sehemu nyingi za kujivinjari kwenye kaunti hiyo hupatikana maeneo hatari, hasa kwa wale ambao kamwe hawajayazoea mazingira ya visiwa.

Utapata sehemu za kutazama samaki wakirukaruka kama vile Manda-Toto na Ras Kitau zikiwa katikati ya Bahari Hindi, hasa maeneo ya kina kirefu.

Kwa wale wanaotaka kuifurahisha nafsi na kuondoa msongo wa mawazo kupitia kulitazama jua likichomoza alfajiri au kutua jioni, utahitajika kupanda boti au mashua kufika eneo la Shela na kukaa katikati ya bahari ya kina kirefu ili uwahi kwa makini mandhari hayo.

Isitoshe, mikahawa ya kipekee iliyojengwa katikati ya Bahari Hindi pia inapatikana Lamu.

Hapa, wageni na watalii wengi wa humu nchini na ng’ambo hukimbilia kufika kwenye mikahawa hiyo ya kuelea katikati ya bahari, wakiamini kuwa ni mazingira hayo ambayo huudhihirisha bayana utamu wa Lamu.

Bi Fridah Njeri, mmoja wa wamiliki wa mikahawa inayoelea baharini kisiwani Lamu, anachacha kuwa ‘Lamu ni Tamu’ ila kuugundua utamu wake lazima uyakubali na kuyadurusu maisha ya baharini.

“Wa Amu tunaamini kuwa ziara ya mgeni au mtalii yeyote eneo hili haiwezi kukamilika bila kuonja maisha ya ubaharia. Kwa mfano, kuzuru sehemu kama hizi za mikahawa inayoelea katikati ya bahari lazima upande boti, mashua au jahazi kuivuka Bahari Hindi ndipo ufike. Hapa ndipo kwenye ule utamu kindakindaki uvumao kuihusu Lamu yetu,” akasema Bi Njeri.

Bw Chrispinus Juma, mmoja wa watalii wa ndani kwa ndani, ambaye pia ni Afisa Mshauri na Mtaalamu wa Mawasiliano kuhusu Masuala ya Mabadiliko ya tabianchi, anasema Lamu ina wenyewe.

 

Bw Juma Chrispinus (katikati) na wenzake wakibembea kwenye behewa au nyavu maalum zilizofungwa ndani ya Bahari Hindi katika upande wa kisiwa cha Pate.  Bw Juma na wenzake ni watalii wa ndani kwa ndani. Anasema Lamu ina utamu wake, ila ni ujue kuogelea. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Juma, ambaye yuko ziarani Lamu, anasifu eneo hilo kwa kuwa mwafaka kiburudani.

Afisa huyo hata hivyo anawashauri wanaofika au wenye nia ya kuzuru visiwa vya Lamu kuwa tayari kujifunza uogeleaji, akishikilia kuwa huenda kwa wakati fulani wakajipata kwenye jazba zinazowahitaji kuwa na mbinu ya uogeleaji.

“Lamu ni tamu ila ina wenyewe. Usipofahamu mapema siri ya kujihami na maarifa ya kuogelea, huenda ukajipata ukiyabugia mafunda ya maji ya Bahari Hindi ambayo ni ya chumvi. Mimi naipenda Lamu,” akasema Bw Juma.

Kwenye maeneo kama vile kisiwa cha Pate kilichoko Lamu Mashariki, pia utapata mabanda ya kupunga hewa yakiwa ndani ya Bahari Hindi.

Kwa yule asiye mwoga wa maji, hapa utapata wasaa wa kujianika kwenye behewa au nyavu maalumu ambayo ni pana na iliyotundikwa juu kwa aina yake ilhali chini kukiwa ni bahari tupu.

Isitoshe, wasioifahamu vyema Lamu, hasa maeneo ya visiwani, lazima watambue kuwa kwa namna yoyote ile, watahitajika kuivuka bahari ili kuvifikia visiwa husika.

Yaani kila kitu Lamu ni maji au bahari tu.

Na ndiyo sababu utapata kuwa hata stesheni za petroli kwenye visiwa vya Lamu hupatikana ndani au katikati ya bahari.

Hicho ni kinyume kabisa na sehemu zingine za nchi, ambapo vituo hivyo vya mafuta hupatikana nchi kavu.

“Huwezi kuvifikia visiwa vyetu Lamu bila ya kuunganishwa kwa usafiri wa majini ambao ni boti, mashua au jahazi. Hiyo inamaana kuwa kwa mwoga wa maji au bahari hawezi kuipata raha asilia ya Lamu,” akasema Bi Rafa Aboud.

Mkahawa wa Floating Bar ukielea katikati ya Bahari Hindi kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU