Habari

Waombolezaji wahepa na maiti

June 13th, 2020 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

MAELFU ya waombolezaji Ijumaa waliponyoka na mwili wa mwimbaji wa nyimbo za Kijaluo maarufu kama Ohangla, Benard Onyango Obonyo, anayefahamika zaidi kama Abenny Jachiga.

Waombolezaji hao waliwazidi polisi nguvu kwa kuwapiga mawe kabla ya kunyakua jeneza mara lilipowekwa ndani ya kaburi tayari kufunikwa kwa mchanga.

Waliweka jeneza hilo kwenye tuktuk na kisha kulibeba hadi katika uwanja ulio karibu na shule ya msingi ya Kadiju ambapo kulikuwa na msongamano mkubwa wakitazama mwili.

Kisha walizunguka kijijini kwa muda wa saa kadhaa wakiwa wamebeba jeneza hilo kabla ya kuupeleka mwili huo katika mochari ya hospitali iliyo karibu ya St Elizabeth Chiga Missionary Hospital.

Ijumaa jioni, duru ziliambia Taifa Leo kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuzika mwili huo usiku baada ya kuitisha usaidizi wa maafisa zaidi kutoka kaunti jirani.

Wakati wa vurumai hizo, waombolezaji hao walipuuza tahadhari zinazopaswa kuzingatiwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Milio ya risasi, vitoa machozi na umati mkubwa ulishuhudiwa kutoka hospitali ya Port Florence katika barabara ya Kisumu-Busia, hadi kijiji cha Kadiju, Kisumu Mashariki ambacho kawaida huwa kimetulia.

Wanakijiji walishuhudia vurumai zilizofanya polisi zaidi ya 30 kushindwa nguvu na umati, na kulazimika kutoroka waombolezaji hao waliokuwa wenye hasira walipoondoa mwili kaburini baada ya polisi kuuteremsha.

Mwanamuziki huyo anaenziwa kwa nyimbo zake na ana mashabiki wengi.

Waombolezaji hao waliziba eneo la kaburi wakitaka mazishi yaahirishwe ili kuwapatia muda wa kumpatia marehemu sherehe inayomstahili kulingana na tamaduni za Wajaluo.

Haya yalifanyika huku viongozi wa kanisa, mkewe na familia wakistaajabishwa na kilichokuwa kikiendelea.

Kulingana na kanuni zilizowekwa na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o za kukabiliana na corona, maiti zafaa kutolewa mochari kabla ya saa tatu na nusu asubuhi na kuzikwa katika muda wa saa sita baadaye.

Pia aliagiza kuwa wafu watazikwa ama kuchomwa katika muda wa saa 48 baada ya kufariki.

Lakini waombolezaji walipuuza kanuni hizo za Gavana Nyong’o na kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho, wake kwa na waume na hata watoto, wakilia, huku vitoa machozi vilivyorushwa na polisi vikiwazidishia machozi.

Baadhi walisafiri kwa pikipiki kutoka Homa Bay, Kericho na kaunti nyingine ndogo za Kisumu kila mmoja akitaka kushuhudia mazishi hayo.

Shangazi yake marehemu, Bi Linet Muga, alisema marehemu alikuwa kinyozi kabla ya kupata umaarufu wake kimuziki.