Habari Mseto

Wapenzi wa M-Pesa sasa kutuma hela moja kwa moja hadi Uchina

December 1st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WATUMIZI wa M-Pesa sasa wanaweza kutuma pesa moja kwa moja hadi Uchina kwa kutumia mtandao mkubwa zaidi nchi humo, WeChat.

Biashara hiyo imewezeshwa na Family Bank ikishirikiana na SimbaPay, ambayo ina makao yake jijini London.

Ili kutuma pesa, Wakenya watatumia nambari ya kutuma inayomilikiwa na Family Bank ambapo namba ya simu ya wanaotaka kutumia ndio nambari ya akaunti.

Mpokeaji atapata pesa hizo katika mfuko (wallet) wa simu yao. Gharama kutuma itakuwa tofauti kuambatana na kiwango cha pesa ulichotuma. Kwa mfano, kutuma Sh8,198 itagharimu Sh350.

“Hatua hiyo ni kubwa kwetu na kwa wateja, tunataka kuwapa wateja wetu huduma ambayo wanaweza kutegemea ili kutumia washirika wao wa kibiashara China pesa kwa njia wanayoweza kufuatilia,” alisema afisa mkuu wa operesheni Family Bank Godfrey Kamau.

Pia, wateja wanaweza kutumia PesaPap au huduma ya ujumbe kwa nambari iliyotambulishwa na benki hiyo kutuma pesa kwa WeChat.