Habari Mseto

Wapigakura Mwingi Kaskazini walimeza hongo – Munuve

March 20th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Mbunge wa Mwingi Kaskazini John Munuve  ameomba mahakama ya rufaa ibatilishe uchaguzi wa Bw Paul Musyimi Nzengu akidai shughuli ya uchaguzi ilikuwa na dosari tele.

Bw Munuve alisema alidhulumiwa kwa matumizi ya lugha ya kikabila na hata kukejeliwa.

Bw Munuve aliwasihi majaji watatu wa mahakakam ya rufaa wafutilie mbali ushindi wa Bw Nzengu kwa vile ulikumbwa na kasoro nyingi na sheria za uchaguzi zilivunjwa kiholela.

Mlalamishi huyo aliyewania kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Jubilee alisema wapiga kura walipewa hongo na kwamba ukweli ulifichwa.

Bw Munuve aliomba mahakama ikague upya uamuzi wa Jaji Lilian Mutende ambaye alidaiwa hakuzingatia ushahidi kwa makini alipotupilia mbali usahahidi aliowasilisha.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita Bw Nzengu alipata kura 15, 702 ilhali Bw Nzengu alitwaa ushindi kwa kupata kura 23,582.

Mahakama ilifahamishwa wakati wa kampeni wapigakura walikuwa wanashawishiwa kutopigia kura chama cha “Wagikuyu” na badala yake wapigie chama cha “Wakamba”.