Habari Mseto

Wapigambizi kutoka Afrika Kusini wafika kwa uopoaji

October 8th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

WAPIGAMBIZI kutoka Afrika Kusini waliwasili nchini Jumatatu ili kusaidia katika uopoaji wa miili ya Bi Mariam Kighenda na mwanawe waliotumbukia baharini katika kivuko cha Likoni Feri.

Kikosi hicho kilihusisha wapigambizi watano waliokodishwa na familia ya Bi Kighenda na watatu waliokodishwa na serikali ya Kenya.

Walipigwa jeki na wenzao kutoka kikosi cha jeshi cha wanamaji kutoka India.

Matumaini ya kupata miili ya wawili hao yaliongezeka baada ya serikali kununua vifaa maalum vyenye uwezo wa kuona chini ya bahari.

“Tuna matumaini kuwa shughuli hii itakamilika hivi karibuni kwani wataalamu wenye tajriba ya hali ya juu watafanya kazi na wenzao wa hapa nchini wakitumia Kamera zenye uwezo mkuu wa kuona sakafu ya bahari,” alisema mwenyekiti wa shirika la huduma za feri Dan Mwazo.

Mwenyekiti huyo akihutubia wanahabari katika kivuko cha Likoni Feri Mombasa, alieleza serikali imechukua hatua hiyo ili kuongeza nguvu na maarifa ili kuharakisha shughuli ya kutoa miili ya Bi Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu waliozama baharini Septemba 29.

Alieleza kuwa wanatarajia vifaa zaidi kuwasili leo vitakavyosaidia katika juhuda za kutafuta mili.

Siku ya Jumapili Kanali wa jeshi la wanamaji nchini Lawrence Gituma alisema vifaa walivyonavyo kwa sasa japo ni vizuri havina uwezo wa kuona chini ya bahari.

Bw Gituma alisema vifaa hivyo vinavyoendeshwa na kitanzambali vitatumika badala ya wapigambizi kutambua sehemu halisi lilipo gari la mwendazake Bi Kighenda.

“Sehemu ambazo tunatafuta miili wakati huu zina kina kirefu mno; kuna hatari ya wapigambizi kuishiwa na pumzi kisha kufariki, vifaa hivi tutavitumia kutambua gari kabla ya kutuma wataalamu wetu kwenda kuopoa miili,” alisema Kanali huyo.

Toyota

Bi Kighenda na mwanawe walizama wiki iliyopita baada ya gari lao aina ya Toyota ISIS lenye nambari ya usajili KCB 289C kuteleza kutoka feri Mv Harambee na kutumbukia ndani ya maji.

Shughuli ya uopoaji inaendelezwa na shirika la utoaji huduma za feri (KFS), mamlaka ya bandari (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini (KCGS) na taasisi ya utafiti wa baharini.

Shughuli hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo hali mbaya ya hewa,mawimbi makali baharini, giza na kukosa vifaa muafaka vya kuzama kwenye vina virefu.

Wiki iliyopita waokoaji wawili binafsi walijitoa kushiriki katika mchakato huo.

Mswidi Bw Volker Bassen na Musa Sila kutoka humu nchini japo waliruhusiwa kushiriki katika operesheni ya uopoaji chini ya kikosi cha Jeshi la wanamaji la humu nchini walijitoa kabla ya shughuli kukamilika.

Bw Bassen alifutilia mbali kauli yake ya kwanza kuwa angeweza kutambua na kuopoa miili ya Bi Kighenda na mwanawe kwa muda wa masaa mawili.

“Naomba familia na Wakenya msamaha, sikutambua hali halisi ya shughuli hii, sehemu inayoendelezwa operesheni hii ina kina kirefu mno, mawimbi makali, giza na ni makao ya papa,” alisema.