Wapiganaji waua 25 DRC mkesha wa mwaka mpya

Wapiganaji waua 25 DRC mkesha wa mwaka mpya

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

RAIA 25 wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), maafisa walisema Ijumaa jioni.

Walielekeza kidole cha lawama kwa kundi la wapiganaji wa ADF ambalo limekuwa likisababisha visa vya utovu wa usalama eneo hilo.

Wanajeshi walikuwa wakiwakimbiza wapiganaji wa ADF walipokumbana na maiti ya raia hao baada mkesha wa Mwaka Mpya, Donat Kibuana ambaye ni msimamizi wa eneo la Beni Kaskazini wa mkoa wa Kivu Kaskazini aliambia AFP.

Duru zilisema kuwa mauaji hayo ya kikatili yalitekelezwa katika kijiji cha Tingwe, kilichoko umbali wa kilomita nane kutoka mji wa Eringeti.

Hata hivyo, mshirikishi mkuu wa makundi ya mashirika ya kijamii, Tingwe, Bravo Mohindo Vukulu alisema idadi ya waliofariki ilifikia 30 kulingana na takwimu zao zilizotolewa jana asubuhi.

“Watu walikuwa wameenda katika mashamba yao kujiandaa kukaribisha Mwaka Mpya, kabla ya wapiganaji wa ADF kuwashambulia mmoja baada ya mwingine,” akasema.

“Tuliwapasha habari wanajeshi wa serikali kuhusu uwepo wa wapiganaji wa ADF katika eneo zima la Eringeti. Lakini hawakuchukua hatua ya kufika kwa haraka,” Vukulu akaongeza.

Kundi la ADF, ambalo lilichipuza katika miaka ya 1990s ni mojawapo ya zaidi ya makundi 10 ya wapiganaji nchini DRC.

Limelaumiwa kwa vifo vya zaidi ya raia 800 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika mkoa wa Kivu Kaskazini, unaopakana na Uganda.

Kundi hilo la wapiganaji huchuma fedha kupitia ulanguzi wa mbao kutoka taifa hilo lenye eneo kubwa la misitu ya kiasili. Maafisa wa DRC wanashuku kuwa huenda baadhi ya wanajeshi ni washirika katika visa hivyo vya mashambulio.

Hata hivyo, uongozi wa ADF haijawahi kudai kuhusika katika mashambulio hayo.

Lakini tangu Aprili 2020 kundi moja la wapiganaji wa Kiislamu nchini humo lilidai kuhusika na mashambulio hayo, japo halikutoa ithibati.

Mnamo Julai, mwaka jana, Umoja wa Mataifa (UN) ulitaja mashambulio ya kundi la ADF kama uhalifu dhidi ya kibinadamu na uhalifu wa kivita.

Wakati huo huo, idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Chalane kati mwa Musumbuji imepanda kutoka wanne hadi saba, kulingana na Shirika la Kushughulikia Majanga nchini humo (INGC).

Kimbunga hicho pia kiliathiri sehemu kadha Madagascar na Zimbabwe.

You can share this post!

Wasanii mashuhuri waliofariki 2020 hivyo kuacha pengo kubwa...

Wakazi sasa wataka daraja liwekwe kivuli kuzuia jua