Habari Mseto

Wapigapicha waambulia makombo wenye mitambo ya kisasa ‘wakiharibu’ soko

January 1st, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

WAPIGAPICHA na watengenezaji filamu huvuna siku ya kwanza ya kufungua mwaka kutokana na msimu ambao huwa na sherehe kemkem.

Hata hivyo, mara hii katikati mwa mji la Nairobi na bustani ya Uhuru Park ni kinyume na matarajio kwa wapigapicha na watengenezaji filamu ambao wanalilia athari ya ‘soko huru’ pamoja na idadi ya ndogo ya wateja.

Christopher Njihia anaambia Taifa Leo Dijitali, kuwa tangazo la kuondolewa kwa malipo ya bustani hiyo na serikali ya Kaunti ya Nairobi lilimweka ari ya kufanya kazi kubwa Januari 1, 2024. Alifika mwendo wa saa tatu asubuhi lakini kufikia saa tano, ni mteja mmoja pekee alikuwa amepata.

“Leo ni tofauti na mwaka jana. Ni mteja mmoja ambaye amelia na kunilipa Sh80 kwa picha mbili. Pia, tuko wengi kila mmoja anakazana kupata riziki yake na bei yake. Hatuna kiwango sawa hapa,” alisema Bw Njihia.

Mpiga picha mwenye umri wa makamo alikuwa amesimama muda mrefu kwenye bustani hiyo, akisema wateja wengi wanahitaji upiga picha wa kisasa na kukataa ule wa kitambo.

“Siku hizi si rahisi kupata wateja. Watu wengi wanapendelea upigaji picha wa kisasa unaofanywa na vijana. Tunauita mtindo wa milenia wa upigaji picha,”alielezea.

Katikati mwa jiji kuu vijana mbalimbali wanafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa wanapata wateja wao.

Samuel Warui ni mpigapicha mwingine wa zaidi ya miaka 3. Anasema sheria ya kuwepo kwa soko huru imesababisha hasara msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya.

“Aliye na ujuzi au hana, wote tumo hapa. Hii barabara ya Avenue, kuna wapigapicha tisa,” alisema Bw Warui.

Bw Warui ambaye hutegemea wateja wake kuwa familia, sherehe za harusi, RuracioBabyshower na kuzaliwa, alisema bei ya kupiga picha imepungua pia kutokana na ugumu wa maisha.

“Nimekuwa na mteja wangu ambaye kila mwezi alilipa Sh3,000 baada ya kazi. Msimu huu wa Krismasi na Mwaka Mpya alionekana mara moja. Mteja huyo ana kazi ya hadhi ya juu, na nimefanikiwa kumpata mara moja tu. Wakati walikuja aliniambia gavana– jina la utani, leo nataka unipige picha za Sh1,000,” aliongeza Bw Warui.

Mpiga picha huyo na wenzake katika barabara hiyo wana kiwango sawia cha kulipisha picha wanazozipiga japokuwa kuna wale ambao hawana taaluma hiyo. Na hivyo kuharibu bei ya picha mjini.

“Wateja wangu huwa vijana ambao wameajiriwa, wanaofanya kazi, familia lakini sio wanafunzi. Unapata wezangu wanapiga picha tu kuchukua kile wanalipwa wakijua kuwa wazazi watawalipia kodi ya nyumba. Mimi nikipata Sh200 kwa siku nitaridhika nayo lakini wasio na taaluma hii labda mzazi alinunua kamera basi atachukua hata Sh50,” alinung’unika Bw Warui.

Septemba 2022, Gavana wa Kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja aliwaondolea malipo ya vibali vya biashara kwa wapigapicha na watengenezaji filamu wa kujitegemea wanaohudumu ndani ya kaunti hiyo.

Gavana Sakaja alifanya marekebisho ya sheria ‘za kale’ ambazo zilikuwa zikizuia upigaji picha, video, filamu na tasnia pana ya ubunifu jijini Nairobi.