Habari Mseto

Wapigeni risasi wanaoharibu miundo misingi- Kindiki

March 11th, 2024 1 min read

NA PIUS MAUNDU

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amewaamuru polisi kupiga risasi na kumuua mtu yeyote anayepatikana akiharibu Reli ya Standard Gauge (SGR) na miundomsingi mingine muhimu kote nchini kama vile Sasumua, Ndakaini na bwawa linayolengwa la Thwake.

Akizungumza wakati wa kuzindua Naibu Kamishna Teresia Mburu kufuatia kuchapishwa katika gazeti la serikali kwa Kaunti Ndogo ya Kambu, Kaunti ya Makueni wiki tatu zilizopita, Prof Kindiki alitoa onyo kali kwa wanaoharibu miundombinu muhimu ili kuuzia wafanyabiashara wa vyuma vikukuu akisema siku zao zimehesabiwa.

“Tumechapisha kwenye gazeti la serikali sheria mpya inayolinda reli na miundombinu mingine muhimu. Mtu yeyote anayepatikana ndani ya eneo la kituo kilichohifadhiwa, kama vile reli na mabwawa ya maji, atashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa. Hiyo ndiyo sheria na ina adhabu. Ni sheria hii inayolinda Ikulu. Sheria inaruhusu afisa wa polisi kusafirisha mara moja hadi kuzimu mtu yeyote anayepatikana ndani ya eneo lililohifadhiwa bila kuwakamata,” Prof Kindiki alisema kwa mafumbo Jumatatu, Machi 11, 2024.