Wapingao BBI wataka rufaa isikizwe na majaji 11

Wapingao BBI wataka rufaa isikizwe na majaji 11

Na JOSEPH WANGUI

WALALAMISHI katika mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) wanataka rufaa zitakazowasilishwa na wale wanaounga mkono mchakato huo kusikilizwa na majaji 11.

Kupitia chama cha Thirdway Alliance na mwanauchumi David Ndii, walalamishi hao wanaomba rufaa ya kusitisha kuharamishwa kwa mchakato wa BBI, isikilizwe kwa siku mbili.

Kwenye barua mbili walizowasilisha kwa kiongozi wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Daniel Musinga, walalamishi hao wanataka majaji hao kusikiliza kesi hiyo na wapewe muda zaidi, kwani kesi hiyo ni yenye uzito na inawahusisha watu wengi.

“Tunaomba kesi hii kusikilizwa angaa na majaji saba kutokana na uzito wake na masuala yanayorejelewa. Hili pia linatokana na umuhimu wa kesi hiyo kwa nchi,” akasema wakili Elias Mutuma, anayeiwakilisha Thirdway Alliance.

Pamoja na wakili mwenzake, Nelson Havi, wawili hao walisema kuwa ikizingatiwam kuwa kesi walizowasilisha katika Mahakama Kuu zilisikilizwa na majaji watano, itakuwa vizuri rufaa hizo kusikilizwa na majaji zaidi.

Wanasema majaji wengi watatoa uamuzi bora kuhusu rufaa hizo. Miongoni mwa wale waliowasilisha rufaa hizo ni Mwanasheria Mkuu, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Sekretariati ya BBI, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta aliwasilisha rufaa hiyo kupitia wakili Waweru Gatonye. Rais amekita rufaa yake katika sababu tisa, akikosoa uamuzi uliotolewa na majaji watano, wakiongozwa na Jaji Joel Ngugi.

Kwenye stakabadhi hizo, Rais anasema “amewasilisha rufaa hiyo kwa sababu yeye ni miongoni mwa wale walioathiriwa na uamuzi huo”.

Rais pia anaeleza kutoridhishwa na uamuzi huo. Mahakama iliamua kwamba alipaswa kujibu kesi hiyo yeye binafsi ama wakili wake mwenyewe.

Ilisema hapaswi kuwasilisha rufaa hiyo kupitia Mwanasheria Mkuu. Rais Kenyatta pia ameeleza kutoridhishwa na uamuzi wa majaji kwamba amevunja Sehemu ya Sita ya Katiba.

Vilevile, anapinga uamuzi kuwa kulingana na sheria, hana mamlaka yoyote ya kuanzisha mchakato wa kuifanyia mageuzi Katiba.

Rais pia anapinga uamuzi kuwa mpango wowote wa kuifanyia mageuzi Katiba unaweza tu kuanzishwa na Rais kupitia Mwanasheria Mkuu katika Bunge la Kitaifa, kulingana na Sehemu 256 ya Katiba.

Mbali na hayo, anapinga uamuzi wa majaji kuwa Jopo la BBI lilibuniwa bila kuzingatia taratibu za kisheria.

Wakati huo huo, Bw Odinga anataka Mahakama ya Rufaa iruhusu kufanyika kwa kura ya maamuzi kuhusu BBI, wakati kesi ya kupinga mchakato huo inapoendelea kusikizwa.

Kwenye ombi ambalo Bw Odinga ameandaa kuwasilisha ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, anasema shughuli hiyo isipoendelea itatumbukiza Kenya kwenye mgogoro wa kikatiba.

Kulingana na nakala zilizoandaliwa na wakili Paul Mwangi kwa niaba ya Bw Odinga na sekretariati ya BBI, shughuli hiyo ina umuhimu mkubwa wa kikatiba na hivyo inabidi iendelee kama ilivyopangwa.

“Shughuli ya kubadilisha Katiba ina kazi nyingi kwani ina muda mahsusi unaofaa kuzingatiwa. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa nia ya walioanzisha mchakato huu inaheshimiwa,” anasema Bw Odinga katika ombi lake.

Anasema Wakenya watapata hasara kubwa iwapo Mahakama ya Rufaa haitabatilisha uamuzi wa majaji uliosimamisha mchakato huo. Anataja faida sita za moja kwa moja zilizo kwenye mswada huo kuwa pesa za Serikali za Kaunti, Hazina ya Maeneo Bunge (NG-CDF), Hazina ya Wadi, Vijana na kupunguza ufujaji wa pesa za umma.

“Mswada wa BBI ulilenga kurekebisha kifungu cha 203(2) cha Katiba ili mgao wa pesa kutoka Serikali ya Kitaifa hadi zile za kaunti kufikia asilimia 35 badala ya asilimia 15. Ilitaka kuhalalisha hazina ya CDF itambuliwe na Katiba na kuwafaa wananchi,” inasema sehemu ya rufaa hiyo.

You can share this post!

Korti yacharaza Uhuru kiboko mara nyingine ikisema alipuuza...

Waombaji wasiotenda