Habari

Wapinzani wa Kenya mechi za kupigania tiketi ya Afcon 2021 wabainika

July 19th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars ya Kenya imekutanishwa na washindi wa mataji mengi ya Kombe la Afrika (AFCON) Misri katika mechi za kufuzu kushiriki makala ya 33 nchini Cameroon mwaka 2021.

Vijana wa Sebastien Migne pamoja na Mafirauni hao, ambao ni wenyeji wa makala ya 32 ya AFCON yanayokamilika leo Ijumaa usiku, wako katika Kundi G. Timu za Sparrowhawks ya Togo na Coelacantes ya Comoros zinakamilisha orodha ya washiriki watakaowania tiketi mbili zilizoko mezani kutoka kundi hili.

Kenya itaanza mechi zake Novemba 2019.

Baadhi ya nyota watakaonogesha katika kundi hili ni kiungo wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama (Kenya), mchana-nyavu matata wa Liverpool Mohamed Salah (Misri), mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Adebayor (Togo) na mvamizi wa Red Star Belgrade El Fardou Ben Nabouhane (Comoros).

Rekodi ya Kenya

Kenya ina rekodi mbaya sana dhidi ya mabingwa mara saba Misri. Tangu zikutane mara ya kwanza mwaka 1972, Kenya imeshinda Misri mara moja pekee katika mechi 19.

Timu hizi zimetoka sare mara nne, huku Misri ikikanyaga Kenya mara 14 ikiwemo katika mechi tano zilizopita kwa jumla ya mabao 13-1 ambazo zilikuwa za kirafiki. Ushindi wa Kenya dhidi ya Misri ulipatikana Juni 1 mwaka 1979 wakati ilitamba 3-1 jijini Nairobi katika mechi ya raundi ya tatu ya kufuzu kushiriki AFCON.

Ilibanduliwa nje baada ya kuchapwa 3-0 nchini Misri.

Kenya na Togo zimewahi kukutana mara tano. Kila mmoja anajivunia ushindi mara mbili katika mechi za kufuzu kushiriki AFCON, huku wakitoka sare katika mechi za Kundi A za AFCON mwaka 1972.

Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Comoros katika mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kushiriki AFCON ni mwaka 2015. Stars ililemea wanavisiwa hao 1-0 kupitia bao la Johana Omolo katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Mei 18 mwaka 2014 jijini Nairobi kabla ya kukabwa 1-1 mjini Mitsamiouli katika mechi ya marudiano ambayo Ayub Timbe alifungia timu yake ya Kenya.

Katika mechi ya mwisho ambayo mataifa haya mawili yalikutana mnamo Machi 24 mwaka 2018, Kenya pia ilikabwa 2-2. Ilikuwa ya kirafiki. Ilichezewa mjini Marrakech nchini Morocco.

Licha ya Wakenya kuamini Comoros ndiyo kitoweo katika kundi hili, ukweli ni kuwa wanavisiwa hao si wachache.

Ingawa hawakufuzu kuwa nchini Misri kwa AFCON 2019, Comoros hawakupoteza katika ardhi yao baada ya kukaba miamba Cameroon 1-1 na Morocco 2-2 na kubwaga Malawi 2-1 mjini Mitsamiouli.

Misri inajivunia rekodi ya ushindi sita, sare moja na kupoteza mara moja dhidi ya Togo kwa hivyo kwa jumla Mafirauni wataanza kampeni za kuingia AFCON 2021 na asilimia kubwa ya kufuzu kutoka kundi hili.

Kenya itakuwa ikitafuta kushiriki makala mawili ya AFCON kwa mipigo, kitu ambacho imewahi kufanya mara moja katika historia yake ilipoingia makala ya mwaka 1988, 1990 na 1992. Makala mengine ya AFCON ambayo Kenya imeshiriki ni mwaka 1972, 2004 na 2019.

Togo itakuwa ikitafuta kurejea AFCON baada ya kukosa makala ya mwaka 2019 huku nayo Comoros itafukuzia kuingia mashindano haya kwa mara yake ya kwanza kabisa.

Idadi

Mataifa 52 yatapigania tiketi 23 za kujiunga na wenyeji Cameroon katika AFCON 2021. Cameroon pia itashiriki mechi hizi za kufuzu, lakini kuzitumia kujipima nguvu. Timu moja pekee kutoka Kundi F linalojumuisha Cameroon, Cape Verde, Msumbiji na Rwanda.

Liberia italimana na Chad kuingia mechi za kufuzu za Kundi A, Sudan Kusini ivaane na Ushelisheli kuingia Kundi B, Mauritius na Sao Tome & Principe zikabiliane kuingia Kundi C naye mshindi kati ya Djibouti na Gambia atatiwa katika Kundi D.

Washindi wa makundi yote 12 pamoja na watakaomaliza katika nafasi ya pili watajikatia tiketi ya kushiriki AFCON mwaka 2021.