Kimataifa

Wapinzani waenda mafichoni wakihofia kunaswa na serikali

August 1st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

HARARE, Zimbabwe

WAFUASI kadha wa upinzani nchini Zimbabwe wameenda mafichoni baada ya wenzao kukamatwa kwa kushiriki maandamano ya kupinga serikali, chama kikuu cha upinzani, Movement for Democratic Change (MDC), kimeeleza.

Serikali ilipiga marufuku maandamano makubwa yaliyoitishwa na upinzani kulaani kukithiri kwa ufisadi na kuzorota kwa uchumi.

Idara ya Polisi ilisema maandamano hayangeruhusiwa kuendelea chini ya kanuni na masharti ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 yanayoendelea kutekelezwa.

Serikali imeonya waandamanaji kwamba watachukuliwa kama waliotekeleza kosa la uhaini na hivyo kuadhibiwa vikali kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.

Barabara zilisalia bila watu na biashara zikafungwa katika miji mikuu ya Zimbabwe, Harare na Bulawayo, Ijumaa baada ya vikosi vya usalama kutumwa kuzuia maandamano hayo yaliyoitishwa na viongozi wa upinzani na makundi ya wanaharakati.

“Waandamanaji hawakujitokeza,” Joho Sikhala, ambaye ni mbunge wa upinzani na mmoja wa waandalizi, alisema.

“Uwepo wa maafisa wengi wa usalama unaonyesha kuwa serikali inaogopa raia wake. Lakini maandamano ya kila siku ndio suluhu kwa changamoto zinazoikabili Zimbabwe,” akaeleza.

Sikhala ni miongoni mwa zaidi ya watu 10 ambao wamejificha baada ya kupata habari kwamba wanasakwa na polisi kwa kuandaa maandamano hayo ambayo yaliratibiwa kufanyika Ijumaa.

Mjini Bulawayo na kati mwa jiji kuu, Harare, biashara zote zilifungwa huku polisi na wanajeshi wakishika doria katika barabara kadha.

Hali sawa na hiyo pia ilishuhudiwa katika miji mingine iliyoko viungani mwa Harare, kama vile Mbare, ambao umewahi kushuhudia maandamano makubwa miaka ya nyuma.

Rais Emmerson Mnangagwa aliwafananisha waandamanaji hao na “magaidi” ambao lengo lao ni kuchochea mapinduzi dhidi ya serikali yake.

Chama chake, ZANU-PF wiki hii kilimtaja balozi wa Amerika nchini Zimbabwe, Brian Nicholas, kama “jambazi” kikidai ndiye anafadhili uasi dhidi ya serikali ya Rais Mnangagwa.

Nicholas ameishutumu serikali kwa kufeli kupambana na ufisadi na kwa kuwaandama viongozi wa upinzani, “bila sababu.”

Viongozi wa upinzani wanaisuta serikali kwa kurejelea udikteta wa enzi za Rais wa zamani marehemu Robert Mugabe kwa kuzima maandamano na kuwakamata wakosoaji wake.

Wananchi wamekerwa na kuzorota kwa uchumi kufuatia kupanda kwa mfumko wa bei kwa kima cha zaidi ya asilimia 700, uhaba wa sarafu za kigeni huku hospitali zikizongwa na migomo na uhaba wa dawa.

Msemaji wa polisi, Paul Nyathi, alisema msemaji wa chama kikuu cha upinzani Bi Fadzayi Mahere na mwandishi wa riwaya Tsitsi Dangarembga ni miongoni mwa watu watano waliokamatwa kwa kuchochea fujo baada ya kuongoza maandamano katika mitaa wanakoishi.