Ruto ataka wapinzani waje na sera zao

Ruto ataka wapinzani waje na sera zao

Na WYCLIFFE NYABERI

NAIBU Rais William Ruto jana Jumatatu alitumia ziara yake katika Kaunti ya Nyamira kuwakosoa viongozi wa upinzani kwa madai ya kushindwa kumtambua atakayemenyana naye kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Badala yake, Dkt Ruto alisema viongozi hao wamejikita kwenye ukosoaji wa falsafa yake inayolenga kuinua maisha ya Wakenya kuanzia viwango vya chini maarufu kama Bottom up na kuwataka waje na sera zao za kuwauzia Wakenya.

“Badala ya kusikizana na kutuambia ni nani tutakayeshindana naye, wanazunguka wakikosoa mfumo wa Bottom Up. Waachane na sera zetu na waje na zao za kuwauzia Wakenya. Nataka kuwaambia hawa watu waache kiburi, fitina na madharau,” Dkt Ruto akaambia umati katika masoko ya Keroka na Kijauri akiwarai wapigakura wampe nafasi ya kuongoza taifa.

Naibu Rais aliwaeleza Wakenya kuwa wanaolenga kumenyana naye wamewahi kupata nafasi kuhudumu serikalini lakini akadai hawana rekodi za maendeleo za kuonyesha.

“Yule mwingine alikuwa waziri mkuu, mwingine akawa makamu wa rais, mwingine alikuwa naibu wa waziri mkuu, wapi kazi yao ya kuonyesha watu wa Nyamira? Ikiwa mlishindwa kufanya kitu mkiwa serikalini, mtafanya nini mkiwa mmehitimu umri wa miaka 80?” Dkt Ruto akauliza.

Kuhusu mchakato uliolenga kubadilisha katiba lakini ukaanguka maarufu kama BBI, Naibu Rais alidokeza mswada huo ulipania kumzimia ndoto yake ya kuwa rais wa tano wa Taifa la Kenya lakini akajanjaruka.

Dkt Ruto alionyesha imani atakitwaa kiti cha urais na kuingia Ikulu ya Nairobi.

“Wale wangwana si mliona jinsi walivyonipangia? Walikuja na Reggae nikawaambia itakwama. Si ilizima? Lakini hawakujua kwamba pia mimi nimejipanga sawa sawa. Safari hii watajua hawajui,” Dkt Ruto akaongeza.

Katika eneo la Chepilat, Naibu Rais aliwapongeza wenyeji wa mji huo unaopakana na kaunti za Nyamira na Bomet kwa kuishi kwa amani na kuwataka wadumishe undugu hata kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mji huo ulishuhudia machafuko ya kikabila kwenye uchaguzi wa 2007.

Kama kawaida, Dkt Ruto alichukua fahari kwenye ufanisi wa miradi mbali mbali ya serikali na kusema ni juhudi zake za pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.

Miradi aliyosema Naibu Rais imefaidi watu wa Nyamira ni barabara za lami, kuunganisha wakazi na umeme, ujenzi wa vyuo anuwai miongoni mwa miradi mingine.

Aliwaomba vijana ambao hawajajisajili kama wapigakura kuhakikisha wamepata kadi hizo kabla ya usajili kufika kikomo hii leo Jumanne.

Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi alimlaumu waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kwa kile alisema aliangusha jamii yake kwa kutowania urais na badala yake akatangaza kumuunga kinara wa ODM Raila Odinga.

“Yule tuliyemdhania atawania urais mliona siku iliyopita kule Mwongori alidokeza atasimama na mtu mwingine. Sisi hatutakubali hayo,” Bw Kemosi akasema.

Mbunge wa Mugirango Kaskazini Joash Nyamoko alisema ni kupitia kwa Naibu Rais na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) ambapo umoja wa Wakenya utapatikana.

Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro alisema jinsi Dkt Matiang’i yuko karibu na Rais Uhuru Kenyatta, vivyo hivyo ndivyo alivyo karibu na Naibu Rais William Ruto.

Alimtaka Rais Kenyatta ahakikishe watu waliohusika kwenye ufujaji wa pesa zilizotengewa janga la corona wanachukuliwa hatua kali.

Viongozi wengine walioambatana na Dkt Ruto ziarani ni mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, mbunge wa Sotik Dominic Koskei, mbunge wa zamani wa Mugirango Kusini Omingo Magara miongoni mwa wengine.

Hii leo Jumanne Dkt Ruto anamalizia ziara yake ya siku mbili Nyamira kwa kuzuru maeneobunge ya Mugirango Magharibi na Mugirango Kaskazini.

You can share this post!

Majaji: Uhuru ashinda raundi ya kwanza

Matiang’i ajibu madai ya wandani wa Dkt Ruto kuhusu...

T L