Michezo

Wapinzani wangu wataisoma namba – Ferguson Rotich

August 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya kusajili matokeo duni kwenye duru ya kwanza ya mbio za Wanda Diamond League jijini Monaco, Ufaransa wiki iliyopita, mwanariadha Ferguson Rotich amesema wapinzani wake sasa wataona vumbi kwenye duru ya pili itakayoandaliwa Stockholm, Uswidi mnamo Agosti 23.

Rotich alitupwa hadi nafasi ya nane kwenye mbio za mita 800 mjini Monaco baada ya kuandikisha muda wa dakika 1:45.48.

Kivumbi hicho kilitawaliwa na bingwa wa dunia Donavan Brazier wa Amerika aliyeandikisha muda wa dakika 1:43.15 baada ya kumpiku Mmarekani mwenzake Bryce Hoppel aliyeridhika na nafasi ya pili kwa muda bora wa dakika 1:43.23. Marco Arop wa Canada alifunga orodha ya tatu-bora kwa muda bora wa binafsi wa dakika 1:44.14.

“Sikuwa nimejiandaa vilivyo kwa duru ya Monaco kwa kuwa ratiba yangu ilivurugwa na virusi vya corona. Sasa niko katika hali shwari ya kutamba kwenye kivumbi cha Stockholm,” akasema Rotich aliyejitwalia nishani ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019.

Ilikuwa mara ya nne kwa Rotich, 30, aliyeandikisha muda wa dakika 1.43.82 jijini Doha kunogesha mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia zilizotamalakiwa na Brazier (1:42.34).

Hiyo ilikuwa medali ya kwanza kwa Rotich kunyakua kwenye Riadha za Dunia. Aliambulia nafasi ya tano mnamo 2013 jijini Moscow, Urusi.

Akishiriki mbio za Diamond League mjini Monaco mwaka jana, Rotich aliambulia nafasi ya pili kwa muda wa dakika 1:42.54 nyuma ya Nigel Amos wa Botswana aliyeandikisha muda wa dakika 1:41.89. Amel Tuka wa Bosnia aliridhika na nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 1:43.62.

Rotich ni miongoni mwa wanariadha wa haiba kubwa ambao wamealikwa kushiriki mbio za Diamond League jijini Stockholm mwishoni mwa wiki hii.

Atatoana jasho na Brazier na Tuka kwa mara nyingine katika mbio za mita 800 ambazo pia zimemvutia mshikilizi wa rekodi ya kitaifa nchini Uswidi, Andreas Kramer.

Kwa upande wa wanawake, Halima Nakaayi ya Uganda atafufua uhasama wake na Raevyn Rogers wa Amerika katika mbio hizo za mizunguko miwili. Wawili hao walitawala fani hiyo katika Riadha za Dunia mwaka jana kwa kuibuka katika nafasi ya kwanza na pili mtawalia.

Mwingereza Jemma Reekie anayejivunia muda bora zaidi wa binafsi wa dakika 1:57.91 pia atakuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha kivumbi hicho.

Nicholas Kimeli amesema atapania kuandikisha muda bora zaidi wa binafsi atakapotifua kivumbi cha mita 5,000 jijini Stockhholm. Kimeli ambaye atakuwa akilenga ushindi wa kwanza kwenye Diamond League tangu 2018, atatoana jasho na mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 miongoni mwa chipukizi barani Afrika, Jacob Krop.

Wawili hao walizidiwa maarifa na bingwa wa dunia katika mbio za mita 10,000 Joshua Cheptegei wa Uganda aliyetumia duru ya Monaco mnamo Agosti 14 kuvunja rekodi ya dunia iliyokuwa imedumu kwa miaka 16 kwenye mbio za mita 5,000.

Bingwa huyo mara mbili wa mbio za nyika za Maria Soti, anajivunia muda bora wa dakika 12:57.20 aliousajili mnamo 2019 katika mbio za Helglo Track.

“Janga la corona limevuruga mengi ya maazimio yangu msimu huu. Hata hivyo, nitajitahidi kuandikisha muda bora nchini Uswidi na ikiwezekana, kuibuka na ushindi wa kwanza katika Diamond League,” akasema Kimeli ambaye pia ni bingwa wa mbio za nyika za Ndalat Gaa.

Amesema makala ya Diamond League muhula huu yatampa jukwaa mwafaka zaidi la kujiandalia kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan iliyoahirishwa hadi mwakani. Kimeli alikuwa sehemu ya kikosi cha Kenya kilichoshiriki Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar mnamo 2019 na akaambulia nafasi ya tano kwenye mbio za mita 5,000.

Baada ya Stockholm (Agosti 23) duru za Diamond League msimu huu zitaadaliwa Lausanne (Septemba 2), Brussels (Septemba 4), Naples (Septemba 17), Doha (Septemba 25) na China (Oktoba 17).