Wapwani si wavivu, Shahbal asema

Wapwani si wavivu, Shahbal asema

Na VALENTINE OBARA

MWANASIASA Suleiman Shahbal, anayepanga kuwania ugavana Mombasa 2022 ametaka Wapwani wapewe nafasi za kujiendeleza kimaisha badala ya kusingiziwa kuwa ni wavivu.

Dhana ya kuwa wenyeji wa eneo la Pwani huwa ni wavivu imekuwepo kwa muda mrefu, na wakati mwingine husemekana kutumiwa kama kisingizio cha kuwanyima nafasi za ajira.

Kulingana na Bw Shahbal, kile ambacho Wapwani, hasa wakazi wa Mombasa wamekosa ni mandhari bora ya kuendeleza biashara ndogo ndogo.

“Mimi ni mfanyabiashara na ninaamini uchumi wetu hutegemea biashara ndogo ndogo. Mojawapo ya ajenda zangu kuu itakuwa ni kustawisha biashara hizo. Watu wetu si wavivu, wanahitaji tu mandhari bora yatakayofanikisha biashara zao. Hawajapata nafasi na usaidizi ambao wanahitaji,” akasema.

Huku akijitetea dhidi ya baadhi ya wanasiasa wanaodai kuna wengine wanaomezea mate ugavana ili wajinufaishe kibinafsi, Bw Shahbal alisema Mombasa inahitaji kiongozi ambaye ana uwezo wa kuleta mabadiliko kimaendeleo kwa kiwango kitakachoboresha maisha ya wananchi.

Katika mahojiano aliyokuwa amefanyiwa awali, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir alitahadharisha umma kuhusu viongozi wanaolenga masilahi yao ya kibinafsi bila kumtaja yeyote.

Mbunge huyo na Bw Shahbal wanatarajiwa kushindania tikiti ya Chama cha ODM kuwania nafasi ya kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho mwaka ujao.

“Mimi natafuta uongozi ili kubadilisha maisha ya watu. Nimejitosa ulingoni kuhakikisha wakazi wa Mombasa wanapata kiongozi anayejali maslahi yao na wala sio wale ambao wamekuwa mamlakani kwa zaidi ya miaka minane lakini kwa sababu ya ubinafsi wao hakuna maendeleo ambayo wamefanyia watu,” akasema.

Hata hivyo, katika mahojiano na Taifa Leo jana, Bw Nassir ambaye amekuwa Mbunge wa Mvita kuanzia mwaka wa 2013, alipuuzilia mbali wanaotilia shaka utendakazi wake, akisema hana muda wa kujibizana nao.

Tofauti na Bw Nassir ambaye anatarajia kutumia mafanikio yake ya ubunge kudhihirishia wapigakura uwezo wake wa uongozi, Bw Shahbal atategemea weledi wake wa kibiashara kushawishi wenyeji kwamba ana uwezo wa kuvutia uwekezaji na kuongeza nafasi za ajira, kando na kuhakikisha kuna usimamizi bora wa rasilimali za kaunti.

Katika eneobunge la Mvita, Bw Nassir hujivunia kuleta maendeleo hasa katika sekta za elimu na afya ambapo amewahi kutuzwa na mashirika mbalimbali kwa matumizi mema ya fedha za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF).

You can share this post!

Mudavadi apuuzilia mbali dai la kuwepo juhudi kufufua NASA

Vinara wa NASA wawakanganya wafuasi wao