Wapwani wakaushwa tena

Wapwani wakaushwa tena

Na WAANDISHI WETU

MASAIBU yanayokumba wakazi wa Pwani wanapojitafutia riziki yanazidi kuongezeka, baada ya kubainika kuwa, wavuvi wanaotegemea Bahari Hindi sasa wanasukumwa nje na meli kubwa za makampuni ya kigeni.

Katika miaka ya hivi majuzi, mifuko ya wakazi wengi wa Pwani imekauka kwa vile sekta zilizokuwa zikitegemewa sana kiuchumi zimedorora.

Sekta ya uchukuzi ambayo kwa muda mrefu ilitegemewa kutoa nafasi za ajira kwa vijana na wawekezaji ilianza kulemewa punde baada ya reli ya SGR kukamilika.

Hali hiyo ilisababishwa na sera ya serikali kuu iliyohitaji mizigo yote inayotoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi isafirishwe kwa njia ya reli.

Safari za SGR ziliathiri uchukuzi wa abiria kwa basi, hali iliyopunguza mapato kwa makampuni ambayo yalilemewa zaidi wakati janga la corona lilipozuka.

Hitaji kuwa magari ya uchukuzi wa umma yapunguze idadi ya abiria kama mbinu ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, lilifanya baadhi ya makampuni kama vile Modern Coast na Mombasa Raha kusitisha uchukuzi wa abiria kwa muda usiojulikana.

Hatua hii iliwaacha mamia ya watu bila ajira.Sekta ya utalii iliyokuwa imeanza kufufuka baada ya kupata pigo kutoka kwa mashambulizi ya kigaidi, ilififia tena wakati wa janga la corona.

Kufikia sasa, hoteli nyingi za Pwani bado zinatatizika kurejelea hali ya kawaida kwa sababu ya hasara zilizopatikana tangu mwaka uliopita huku idadi ya watalii pia ikipungua pakubwa kutokana na changamoto za usafiri kimataifa zinazoendelea kushuhudiwa.

Walioathirika si wamiliki na waajiriwa wa hoteli kubwa kubwa pekee bali pia wafanyabiashara wadogo kwa kuwa kufikia sasa, fuo nyingi za umma zilizokuwa zikivutia watalii wa humu nchini zingali zimefungwa.

Viongozi wa kisiasa Pwani hawana msimamo mmoja kuhusu namna ya kutatua changamoto hizi kwa sababu ya tofauti zao za kisiasa.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho ambaye katika miaka iliyopita alikuwa mstari wa mbele kushinikiza serikali ikomeshe dhuluma dhidi ya Wapwani, alibadili mtindo wake baada ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuamua kushirikiana kupitia kwa handisheki.

Katika hotuba zake tangu wakati huo, Bw Joho husema uamuzi wake wa kukumbatia mashauriano na viongozi wa kitaifa, akiwemo rais, kuhusu changamoto za Wapwani ndizo zimewezesha miradi mikubwa ya miundomsingi kufanikishwa eneo hilo.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasisitiza kuwa, Wapwani bado wanateseka licha ya miradi hiyo mikubwa inayojumuisha ujenzi wa barabara, kutekelezwa na na serikali kuu.

“Nilipokuwa nikizungumzia mambo haya awali, watu walidhani nina wazimu, mimi si wazimu. Tumeingia katika siasa sio eti kwa sababu tunapenda siasa ila tunataka kukomboa watu wetu,’ Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali alisema majuzi.

Licha ya kuwa jamii nyingi Pwani zimetegemea uvuvi kama kitega uchumi tangu jadi, sasa kuna ushindani kutoka kwa meli kubwa zinazotumia mbinu ya kukokota nyavu chini ya maji kuvua samaki.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibainisha kuwa, wavuvi wengi sasa wameamua kuacha kwenda baharini na badala yake hununua samaki kutoka kwa wafanyabiashara Wachina.

Mbali na Wachina, imebainika kuwa meli nyingine kubwa zilizopata leseni kuvua samaki nchini humilikiwa na mashirika kutoka Ushelisheli, Italia, Taiwan, na Hong Kong.

Katika mwaka wa 2020 pekee, meli saba kubwa za Uchina zilisajiliwa kufanya uvuvi katika maji makuu humu nchini na leseni zao zitadumu hadi Desemba 2031.

Samaki sasa huvuliwa na meli hizo kubwa kabla wafike katika sehemu za maji ambapo wavuvi Wakenya walikuwa wakitegemea kwa shughuli zao.

Bw Ngole Mbaji ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa kikundi cha kusimamia wavuvi Mtwapa, Kaunti ya Kilifi alisema, serikali pia imechochea masaibu yao kwa sababu kuna sheria za uvuvi zinazobagua wavuvi wadogo.

“Sasa samaki wote sokoni ni wa kutoka kwa Wachina. Wanawake ambao wanauza samaki huwa lazima waamke alfajiri kwenda katika maghala ya Wachina kununua samaki, wasafishe ndipo wauze,” akasema Bw Mbaji.

Kulingana na Bw Mbaji, serikali kupitia kwa Mamlaka ya kusimamia shughuli za majini nchini (KMA) pia ina masharti mengi yanayogharimu pesa nyingi ambazo wavuvi wanaomiliki meli kubwa ndio wana uwezo wa kugharamia.

Masharti hayo ni kama vile kutafuta cheti cha ukaguzi wa boti mara kwa mara, boti ziwe na ubora unaofikia kiwango cha kimataifa, na waendeshaji boti wapokee mafunzo kutoka kwa taasisi ya Bandari Maritime Academy.

Alisema haya yote yanagharimu zaidi ya Sh100,000 ilhali wavuvi wa Pwani huwa na mapato madogo mno.

“Kile KMA imefanya ni kama kuingiza moshi katika mzinga wa nyuki. Wanatumia udhaifu wetu kutufurusha baharini ili tuwaachie nafasi hawa raia wa kigeni,” akasema Bw Mbaji.

Wale wanaoshindwa kuafikia mahitaji hayo hukamatwa na kushtakiwa.Juhudi zetu kutafuta maoni ya KMA kuhusu suala hili ziligonga mwamba kwani Katibu wa Wizara ya Uchukuzi anayesimamia masuala ya baharini, Bi Nancy Karigithu, na Mkurugenzi Mkuu wa KMA, Bw Robert Njue walikataa kujibu maswali yetu.

Haya yote yanashuhudiwa licha ya jinsi maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya ziara nyingi Pwani wakiahidi kustawisha sekta ya uvuvi.Mojawapo ya ziara hizo ilifanywa Februari na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Bw Peter Munya alipozindua meli tatu kubwa za uvuvi.

Meli hizo zilizokabidhiwa kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa ziligharimu Sh60 milioni na zililenga kusaidia wavuvi wa eneo hilo.

Msimamizi wa kikundi cha wavuvi wa Mtwapa, Bw Ndago Gunga alisema walipokea boti lakini limeegeshwa muda wote huo na wala hawajanufaika nalo.

“Nakumbuka lililetwa katika msimu wa uvuvi. Tulifurahi sana kwa sababu tulitumai kuvua samaki wengi katika maji makuu. Lakini kabla tuanze kulitumia, tukabainisha kuna vifaa muhimu ambavyo havikuwepo ndani. Tulihitajika kuchanga takriban Sh1 milioni ili kulifanyia ukarabati na kiwango hicho ni kikubwa sana kwetu,” akaeleza.

Utumiaji wake pia ungehitaji nahodha aliyehitimu kuliko wavuvi hao, mekanika wa kulifanyia ukarabati kila mara na mafuta mengi.Hali si tofauti kwa wavuvi wa Kaunti ya Kwale.

Mmoja wa wavuvi, Bw Omar Bonga alisema maisha ya wavuvi yamekuwa magumu mno kwani wanalazimika kuchagua kati ya kuinua uwezo wao wa uvuvi au kutunza familia zao kwa pesa kidogo wanazopata.

“Inatubidi kupunguza chakula chetu kila siku kwa sababu pesa hazitoshi. Hali huwa mbaya zaidi tunapohitajika kulipia matibabu au karo za shule,” akasema.

Huku msimu mwingine wa uvuvi ukianza mwezi huu, wavuvi Wakenya wanahofia ni wavuvi wa kigeni pekee watakaoendelea kunufaika.

You can share this post!

MARY WANGARI: Tujihadhari hili zimwi la matumizi ya pufya...

Wakulima wa viazi vitamu walalamikia bei duni