Michezo

Wapwani walalamika kupuuzwa Harambee

May 17th, 2019 1 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIF

BAADHI ya wadau wa soka mkoani Pwani walidai Alhamisi kwamba idadi ya wanasoka kutoka sehemu hiyo waliochaguliwa kwenye timu za taifa zitakazoshiriki katika fainali mbili za bara Afrika yaani AFCON na CHAN, ni wachache mno.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally alisema uteuzi huo haukufanyika kwa njia nzuri hasa umewatenga wanasoka wengi wa Pwani wanaocheza soka ya hali ya juu hapa nchini na ng’ambo.

Baghazally alisema aliyekuwa straika wa Tusker FC, Congo United na Mathare United, Ismail Dunga Manucho ambaye anacheza Ligi Kuu ya Zambia angestahili kuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa cha Harambee Stars kitakachoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON).

Mkurugenzi huyo pia alimtaka kocha mkuu wa Harambee Stars, Sebastien Migne amfikirie winga wa Bandari FC, Shaaban Kenga ambaye mbali na kuwa mkongwe lakini yuko katika kiwango cha juu na ni straika anayeweza kuisaidia timu kufanya vizuri huko Cairo ama kwenye dimba la CHAN.

“Ningemuomba Migne awachaguwe wanasoka wengine kutoka mkoa wetu kwani wako kwenye viwango vya juu na wanaweza kuimarisha timu zetu zote mbili za taifa,” akasema Baghazally ambaye alilaumu uteuzi wa makipa wawili kutoka klabu moja ya Kariobangi Sharks.

Alisema ni jambo la kuhuzunisha kuona golikipa wawili wanatoka timu moja na akadai hiyo ni njia mojawapo ya baadhi ya maofisa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutaka kuhakikisha wachezaji wa timu walizotoka wanachaguliwa na kuwemo kwenye vikosi vya timu za taifa.