Habari za Kitaifa

Waraibu wa Shisha wapata sababu ya kutabasamu

March 29th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

WARAIBU wa Shisha, watengenezaji na wauzaji wa tumbuku hiyo ya maji, wana sababu ya kutabasamu baada ya kubainika kuwa kanuni za kupiga marufuku matumizi na unywaji wa dawa hiyo hazijawekwa sawa kulingana na sheria.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Shanzu Joe Omido alisema hakukuwa na marufuku halali ya Shisha chini ya Kanuni za Afya ya Umma (Udhibiti wa Uvutaji wa Shisha), 2017 kulingana na maagizo ya Katiba.

“Hakuna marufuku halali ya matumizi, utengenezaji, uuzaji au ofa ya uuzaji wa Shisha chini ya kanuni kwa sababu Sheria zilizotajwa hazikuwekwa sawa na Wizara ya Afya ndani ya miezi tisa kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu mnamo 2018,” alisema hakimu.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, kanuni za kupiga marufuku matumizi, utengenezaji na uuzaji wa Shisha zilikoma kutumika baada ya kumalizika kwa muda wa miezi tisa tangu Mahakama Kuu ilipotoa uamuzi wake mwaka 2018.

“Makosa ambayo watu hao 48 walishtakiwa nayo hayapo na washukiwa hawawezi kupatikana na hatia kwa kosa linalotokana na utumiaji wa Shisha,” alisema hakimu huyo alipokuwa akiwaachilia huru watu wote 48 walioshtakiwa kwa kosa hilo.

Hakimu alisema kuwa, yaliyomo kwenye hati ya mashtaka dhidi ya watu 48 inakaidi kifungu cha 134 cha Sheria ya utaratibu wa Makosa ya Jinai, ambacho kinaeleza kuwa shtaka litakuwa na maelezo ya kosa au makosa ambayo mtuhumiwa anashtakiwa nayo.

“Hakuna kosa maalumu katika kesi zilizo mbele yangu kwani makosa hayakuwapo wakati washtakiwa wanadaiwa kukiuka sheria,” alisema.

Hakimu alikataa kukubaliana na mashtaka hayo na kuwaachilia washtakiwa wote na kuamuru warejeshewe dhamana ya fedha taslimu walioweka mahakamani.

Watu hao wote 48 walishtakiwa kwa makosa hayo chini ya Kanuni za Afya ya Umma (Udhibiti wa Uvutaji wa Shisha) za 2017, kwa makosa waliyotenda Januari 14, 2024.

Walishtakiwa kwa kuuza na kuvuta Shisha.

Mahakama Kuu 2018 ilitangaza Notisi ya Kisheria Nambari 292 ya Desemba 28, 2017, ambayo ilipiga marufuku utumiaji wa Shisha kuwa isiyo ya kawaida na kuagiza iratibiwe ndani ya miezi tisa. Hilo halikufanyika.