Warembo na ganda la chungwa

Warembo na ganda la chungwa

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

UNAWEZA ukatumia maganda ya machungwa kwa urembo.

Kukabili tatizo la vinyweleo usoni

Maganda ya machungwa huondoa vinyweleo usoni.

Wanawake wengi hulalamikia tatizo la kutokwa na vinyweleo vingi kwenye miili yao.

Kupambana na hali hii, baadhi yao hutumia wembe ambapo badala ya kuvipunguza, husababisha viongezeke na ngozi za nyuso zao kuzeeka. Badala ya kutumia krimu kali au wembe, maganda ya machungwa yanaweza kukusaidia kuondoa vinyweleo hivyo.

Vinavyohitajika

  • unga wa maganda ya machungwa au malimau kijiko kimoja.

* Unaweza kuandaa unga huo kwa kuyakausha maganda hayo juani kwa siku kadhaa kisha ukayatwanga na kuyasaga kupata ungaunga wake.

  • vijiko viwili vya mafuta ya mzeituni (olive oil)
  • kijiko kimoja cha unga wa mtama
  • kijiko kimoja cha maji ya waridi (rose water)

Namna ya kuandaa

Changanya unga wa maganda ya machungwa au malimau na unga wa mtama kwenye chombo kimoja kisha ongeza mafuta ya mzeituni pamoja na maji ya waridi. Changanya mpaka upate ujiuji mzito.

Jipake ujiuji huo usoni na uache ukae kwa dakika 10. Baada ya hapo, tumia vidole vyako vya mikono kuisugua ngozi yako kwa namna ya kutengeneza mduara. Fanya hivi kwa dakika 10 kisha baada ya hapo, osha uso wako kwa maji safi. Fanya hivyo kila siku kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu na bila shaka utaona mabadiliko.

Tumia maganda ya machungwa kutoa mba kichwani

Watu wengi wanasumbuliwa na ugonjwa wa mba kichwani. Mara nyingi mba hutokea nyakati za baridi kwani kichwa huwa ni kikavu sana kwa kipindi chote hicho. Kama unasumbuliwa na hilo tatizo, unatakiwa kuwa makini na mafuta unayotumia na kuhakikisha unatumia mafuta kila unapoosha nywele zako.

Jinsi ya kufanya

Chukua chungwa ulimenye upate maganda yake. Baada ya hapo, chukua limau likamue kisha uweke kwenye blenda usage hadi uwe na mchanganyiko mmoja.

Matumizi

Osha nywele zako kwanza zitakate na baada ya hapo, zikaushe kisha paka mchanganyiko wako kwenye ngozi. Acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha kwa kutumia shampuu unayotumia ambayo unaamini ni nzuri.

Tumia tiba hii kwa wiki mara tatu na utaona jinsi utakavyokomesha moja kwa moja tatizo la mba kichwani.

You can share this post!

Uhispania wazamisha Uswisi kupitia penalti na kufuzu kwa...

ULIMBWENDE: Unachotakiwa kufahamu kabla ya kutumia...