Habari

Warembo wa Uganda wapiga magoti kumshukuru hakimu baada ya kuachiliwa

July 25th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASICHANA 20 raia wa Uganda Jumatano waliizuzua mahakama ya Milimani, Nairobi kwa kupinga magoti na kumshukuru hakimu mkuu Bw Francis Andayi kwa kuwaachilia huru wakitumia lugha ya Kiganda. “Weballessebo, asante mkubwa,” walisema.

“Bila shaka hawa hawezi kuwa Wakenya. Wasichana wetu hapa nchini hawawezi kufanya haya,” akasema Bw Andayi na kusababisha waliokuwa mahakamani kucheka.

Wasichana hao wote walipiga magoti na kuinamisha vichwa vyao na kuinua mikono wakisema wakitoa shukrani kwa mahakama waliposikia wako huru.

Akiwaachilia wasichana hao Bw Andayi alisema  “kwa moyo wa ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki ninawaachilia na kuwapeana kwa ubalozi wa Uganda nchini warudishwe kwao.”

Ubalozi wa Uganda ulimwandikia hakimu ukimsihi awaachilie ndipo uchunguzi ufanywe kubaini mshukiwa aliyekuwa anataka kuwalangua wasichana hao kuwauza nchini Oman kama wajakazi.

Bw Andayi alisema kuwa wasichana hao walikutwa wameghushi visa ya Kenya katika pasipoti zao.

Wasichana hao walibanduliwa kwenye ndege waliyokuwa wameabiri ya shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) iliyokuwa inaenda nchini Oman.

Wakili wao David Ayuo alisema wasichana hao walikuwa wanalanguliwa na kundi la majangili wanaodai watawatafutia kazi mataifa ya ng’ambo.

“Naomba hii mahakama iwahurumie wasichana hawa wenye umri mdogo kati ya miaka 16-22 waliodanganywa kuna kazi inayowasubiri ng’ambo,” alisema Bw Ayuo.

Alisema walisukumwa na umaskini kutoka nyumbani kwao lakini wakaishia mikononi mwa mikora.